Habari Mseto

Msichoke kutafutia watoto ufadhili wa elimu, wazazi waambiwa

January 20th, 2024 1 min read

NA ALEX KALAMA 

WITO umetolewa kwa wazazi ambao wanatafuta ufadhili wa elimu kwa watoto wao kutembelea afisi husika za serikali na zile za mashirika ya kibinafsi ili kuhakikisha wana wao wanapata haki yao ya masomo.

Mwanaharakati wa kutetea haki za watoto mjini Malindi Helder Lameck amedokeza kuwa Kaunti ya Kilifi iko na idadi kubwa ya watoto wanaohitaji msaada wa kuwawezesha kujiunga na shule za upili.

“Viwango vya umaskini hapa Kilifi bado viko juu kwa sababu ukiangalia familia nyingi, bado zinaishi maisha ya uchochole na nyingine hazimudu hata mlo wa mara tatu kwa siku. Sasa kama kula kwenyewe ni shida, unafikiri familia kama hiyo inaweza kumudu kusomesha watoto kweli?” akauliza Bi Lameck.

Mwanaharakati wa kutetea haki za watoto mjini Malindi Helder Lameck. PICHA | ALEX KALAMA

Kwa upande wake Bi Priscila Dama ambaye ni mzaliwa wa Kilifi lakini mkazi wa Lamu, amewahimiza wazazi wasichoke kutafuta msaada ili watoto wao waliofanya vyema Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE 2023) lakini bado wamesalia majumbani, wapate fursa ya Kujiunga na Kidato cha Kwanza.

“Ninahimiza wale wazazi ambao wako na watoto waliofanya vizuri na wako nyumbani, wasichoke kabisa kutembelea haya mashirika kutafuta msaada,” akasema Bi Dama.

Aliongeza kwamba msaada hautakuja wenyewe nyumbani kwa sababu ni lazima mzazi wajitume kwa kutembelea ofisi mbalimbali bila kupoteza matumaini.