Habari MsetoSiasa

Msifanye mzaha na corona – Raila

April 18th, 2020 2 min read

Na JUSTUS OCHIENG

KINARA wa ODM, Raila Odinga amewaonya Wakenya dhidi ya kupuuza kanuni kali zilizotangazwa na serikali kuzuia ueneaji wa virusi vya corona, huku akisema maradhi haya yapo na yanaweza kusambaa kwa haraka.

Bw Odinga alisema maradhi ya Covid-19 yapo na akawaomba Wakenya kuunga mkono juhudi za serikali za kupambana na ugonjwa huo.

Kinara huyo wa ODM alisema kuwa, hatua ya serikali kupiga marufuku safari zote za ndege za kimataifa, mkusanyiko wa watu zikiwemo ibada makanisani, misikitini, harusi, matanga na hata kueweka kafyu ya kuanzia saa moja jioni hadi saa kumi na moja asubuhi, ni njia za kuwazuia wananchi wasiambukizwe virusi hivyo.

“Rais Uhuru amejaribu sana awezavyo kupiga vita ueneaji wa virusi vya corona, lakini wananchi nao wanafaa pia kusaidia katika harakati hizo. Wakenya wanafaa kuchukua hatua zinazotakikana kumaliza usambazaji,” akasema Bw Odinga.

Alisema haya katika mahojiano na waandishi wa habari, hata baada ya viongozi wa dini kutoka Nyanza kuitaka serikali kufungua makanisa na kuwaruhusu wafanye ibada kwa zamu ili kuhakikisha hakuna msongamano.

Serikali ilikuwa imetangaza kuwa watu 21 kutoka kaunti za Siaya, Kisii, Homa Bay na Nyamira walikuwa tayari wameambukizwa virusi hivyo.

Hata hivyo, viongozi hao wa kidini chini ya Baraza la Viongozi wa Makanisa eneo la Nyanza walimwomba Rais Kenyatta kuondoa marufuku ya watu kutokutana makanisani wakidai kuwa, maombi yatakayofanyika mle ‘yatakemea roho chafu ya janga hili’.

“Pia tumegundua kuwa washirika wengi wamerudi katika dhambi na wamepungua imani kwa kukosa chakula cha kiroho ambacho walipokea kila Jumapili walipohudhuria ibada kanisani,” walisema makasisi hao katika taarifa iliyosomwa na mwenyeketi wa baraza hilo, Dkt Washington Ogonyo-Ngede.

Bw Odinga alisema “ Virusi hivi vya corona si mchezo. Tusivichukulie kimzaha. Tunafaa kubadilisha tabia zetu na kushirikiana na serikali kuzuia kusambaa kwa virusi hivi.”

Aliwaomba Wakenya waache kuilaumu serikali bali waunge mkono masharti makali ambayo yamewekwa kupiga vita usambaaji wa maradhi ya Covid-19.

“Kama mjuavyo, mtu wa kwanza kuambukizwa virusi hivi aliingia nchini kutoka ng’ambo kabla ya viwanja vya ndege kufungwa. Serikali ilifanya jambo la busara kupiga marufuku safari za ndege zote za kimataifa na kwa sasa hakuna haja ya kulaumiana. Hayo yote yalifanyika kitambo na yamepita,” akasema Bw Odinga.

Hata hivyo, alihuzunishwa na vitendo vya baadhi ya watu kama vile naibu gavana wa Kilifi, Gideon Saburi ambaye hakuchukua hatua zilizopendekezwa na kujitenga hata baada ya kurejea nchini, na hivyo kuchangia katika kusambaa kwa virusi hivi.

“Baadhi ya watu hawakufuata mikakati ya kujitenga baada ya kurejea nchini, kama vile naibu gavana huyo wa kaunti ya Kilifi, bali alikutana na watu, akahudhuria mazishi, harusi na pia klabu. Tendo hili lilisababisha kuenea kwa virusi vya corona katika eneo hilo,” akasema.

Aliwasihi Wakenya waendelee kunawa mikono kutumia maji safi na sabuni, wasikaribiane na wakae nyumbani.

Aliongeza kuwa alikuwa katika kamati ya Afrika ya kukusanya misaada ili kusaidia Wakenya maskini hapa Kenya na nchi jirani ama vile Burundi, Burkina Faso, Togo, Gaboni na zingine.

“Pia tunataka kuhakikisha kuwa tunatoa msaada wa matibabu. Pia tunahitaji dola 200,000 kusaidia utafiti katika vyuo vikuu na mashitika mengine kuona kama ‘tutapata dawa’,” Bw Odinga alisema.