Na MACHARIA MWANGI
WAZIRI wa Leba Simon Chelugui ameziomba kampuni mbalimbali zihakikishe kuwa haziwafuti wafanyakazi wao hata zinapokumbatia matumizi ya teknolojia.
“Kama serikali, hatuwezi kupigana au kushindana na matumizi ya teknolojia katika ulimwengu wa kisasa. Hata hivyo, matumizi yake yatekelezwe kwa tahadhari, watu wengi wasipoteze kazi,” akasema. Bw Chelugui akihutubia mkutano wa Mamlaka ya Waajiri kwenye Sekta ya Kilimo Alhamisi.
Waziri huyo alisema kuwa kupoteza kazi enzi hizi ambazo nafasi za kazi pia zimeadimika ni pigo katika jamii, ndiposa kampuni husika zinafaa kujizuia kuwatimua wafanyakazi kwa sababu tu ya ujio wa teknolojia.
“Wizara yangu imekuwa ikishirikiana na Mamlaka ya Mafunzo ya Kiufundi (NITA) kuwapa ujuzi zaidi wale ambao wamepoteza ajira zao ili waajiriwe katika sekta nyinginezo,” akasisitiza waziri huyo.