Msikubali kutishwa na UDA, Uhuru aambia polisi

Msikubali kutishwa na UDA, Uhuru aambia polisi

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amewataka maafisa wa polisi kupuuza vitisho kutoka wanasiasa akiwashauri kuendelea kuchapa kazi kwa ujasiri.

Huku akionekana kujibu madai ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwamba maafisa wa polisi wanafumbia visa vya wapinzani wake kuzua fujo katika mikutano inayoongozwa na Naibu Rais William Ruto, Rais Kenyatta aliwaambia polisi wawe ngangari.

“Nataka kusisitiza tena kwamba msiruhusu vitisho vya kisiasa kuyumbisha utekelezaji wa majukumu yenu kulingana na kiapo chenu. Mwapaswa kutekeleza kazi zenu bila uoga wala mapendeleo na msisikize vitisho kutoka mtu yeyote hata kama ni mwanasiasa,” akasema.

Rais Kenyatta alisema hayo Alhamisi alipoongoza hafla ya kufuzu kwa maafisa wa polisi wa cheo cha inspekta katika chuo cha mafunzo ya Polisi, Kiganjo, Nyeri.

Jumla ya maafisa 288 walifuzu na watatumwa kwenda kulinda usalama maeneo mbalimbali wakati ambapo huduma zao zinahitajika katika udumishaji wa usalama kuelekea uchaguzi mkuu.

Mnamo Jumanne, chama cha UDA kuliandika barua ya malalamishi kwa Rais Kenyatta kikilalamikia kisa ambapo kundi la vijana waliodaiwa kuwa wafuasi wa ODM walivuruga mkutano wa Dkt Ruto katika uwanja wa Jacaranda, eneobunge la Embakasi.

Nakala ya barua hiyo ilitumwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i. Nakala ya barua hiyo pia ilitumwa kwa afisi ya mwendeshaji mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) Karim Khan.

Hata hivyo, msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi  Bruno Shioso alipuuzilia mbali madai ya UDA akisema hayana “msingi na yanalenga kuchafua jina la polisi.”

“Madai yaliyoorodheshwa katika barua hiyo hayana msingi wowote kwani hayajaripotiwa katika afisi zetu,” akaongeza Bw Shioso katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumatano, Januari 19, 2021.

Alhamisi, Rais Kenyatta aliwataka maafisa hao waliofuzu kutekeleza majukumu yao kwa nidhamu na uadilifu.

“Mwajiunga na sekta ya usalama wakati  ambapo tunatekeleza mabadiliko mbali yanayolenga kuimarisha utendakazi. Kwa hivyo, Wakenya watatarajia huduma bora kutoka mwenu kuliko wenzenu waliofuzu hapo awali,” kiongozi wa taifa akasema.

  • Tags

You can share this post!

Kocha wa kike alivyokwea kuwa mkali wa karate

Aunda programu inayotoa huduma za mifugo Afrika Mashariki

T L