HabariHabari MsetoSiasa

Msikubali kutumiwa kutekeleza udhalimu, Ruto awarai polisi

August 20th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amewataka maafisa wa polisi kuendesha wajibu wao kitaalamu na wasikubali kutumika kuendeleza ajenda za kisiasa za watu fulani.

Akiongea Alhamisi alipopokea ujumbe wa vijana na akina mama kutoka maeneo bunge ya Lang’ata na Kibra, Dkt Ruto alisema polisi wanapasa kuwahudumia wananchi na viongozi kitaalamu na sio kwa ukatili.

“Serikali ya Jubilee iliyochaguliwa kidemokrasia inaimani kwa maafisa wa polisi wanaoendesha kazi za kuwahudumia wananchi kitaalamu. Hii ndio maana tuliibadili kuwa kutoka Jeshi la Polisi hadi kuwa Huduma ya Polisi. Huo ndio msimamo wa serikali ya Jubilee,” akasema.

Dkt Ruto alionekana kurejelea kisa cha Jumatatu ambapo maafisa wa kutoka kitengo cha Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) waliwakamata maseneta Cleophas Malala (Kakamega), Steve Lelengwe (Samburu) na Christopher Lang’at (Bomet) kwa kikatili.

Japo polisi walisema watatu hao wakamatwa baada ya kukaidi amri ya kutakiwa kuandikisha taarifa kuhusu makosa mbalimbali waliohusishwa nayo katika kaunti zao, iliaminika kuwa hatua hiyo ilitokana na msimamo wao kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha kwa kaunti.

Alhamisi, Naibu Rais alisema polisi hawafai kutumiwa kuendeleza ajenda za kisiasa kwani hiyo ni kinyume cha Katiba inayowahitaji wao kama watumishi wa umma kutojihusisha na siasa.

“Wanasiasa na watu wengine wanafaa kuendesha mambo yao bila kuwahusisha watumishi wa umma au maafisa wa polisi ambao wajibu wao ni kuwalinda wananchi. Serikali ya Jubilee haiungi mkono sera ya matumizi ya polisi kuendeleza ukatili dhidi ya viongozi na raia,” akaeleza Dkt Ruto.

Mnamo Jumanne Naibu Rais pia alikashifu kukamatwa kwa maseneta hao akisema kitendo hicho kiliiharibia sifa serikali

Kwenye taarifa fupi kupitia kaunti yake ya Twitter Dkt Ruto alisema polisi hawapasi kutumika kuwahangaisha maseneta kutokana na misimamo yao kuhusu suala la ugavi wa fedha kwa kaunti.

“Matumizi ya polisi kudhulumu viongozi kutisha Seneti ni MBAYA. Ama kwa hakika hii sio sababu iliyopelekea Wakenya kuwarauka mapema kutupigia kura,” Dkt Ruto akasema.

Mnamo Jumatano, Waziri wa Usalama Fred Matiang’I alikana madai kuwa yeye ndiye aliamuru kukamatwa kwa maseneta hao kwa lengo la kuhujumu mjadala na upigaji kura kuhusu suala hilo.

“Sina haja yoyote na matokeo ya kura kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha. Suala hilo haliko chini ya wizara yangu bali wizara ya Fedha. Na Idara ya Polisi ni huru na inafanya kazi yake kisheria,” akasema Dkt Matiang’I alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Usalama inayoongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji.

Lakini mnamo Jumatano usiku Gavana wa Nairobi alimwelekezea kidole cha lawama kwa waziri huyo na Katibu katika Wizara yake Karanja Kibicho, akisema wao ndio wanaiharibia sifa serikali.

Alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwaadhibu mawaziri ambao wanaiharibia serikali yake sifa ilhali angependa kuacha sifa nzuri ya uongozi atakapostaafu 2022.

“Mheshima Rais usikubali ujinga huu uendelee. Baba yako alikuwa akiwachapa mawaziri wenye mienendo mibaya; iga mfano wake ikibidi,” akasema Bw Sonko kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen.