Habari Mseto

Msimamo mkali wa Sonko kulemaza shughuli jijini

December 3rd, 2020 1 min read

Na COLLINS OMULO

SHUGHULI katika Serikali ya Kaunti ya Nairobi huenda zikalemazwa hivi karibuni, kufuatia hatua ya Gavana Mike Sonko kukataa kuidhinisha utoaji wa pesa katika akaunti ya kaunti hiyo.

Mtanziko huo wa kifedha kati ya Gavana Sonko na Bunge la Kaunti unaendelea huku serikali ya kaunti hiyo ikishindwa kutekeleza bajeti ya Sh37.5 bilioni.

Wafanyakazi wa baraza la Jiji, madiwani na waajiriwa wa Bunge la Kaunti hawajalipwa mishahara ya miezi miwili iliyopita kwa sababu ya mvutano huo wa bajeti.

Bajeti hiyo ilipitishwa na madiwani mnamo Oktoba lakini Gavana akakataa kuidhinisha Mswada kuhusu Ugavi wa Fedha katika Kaunti ya Nairobi, 2020 na kurejesha tena mswada huo bungeni kupitia notisi rasmi.

Notisi hiyo ilikataliwa baadaye na bunge hilo mnamo Novemba 3, 2020 kabla ya mswada huo kuchapishwa rasmi kama sheria wiki moja baadaye baada ya gavana huyo kukataa kutia sahihi yake katika bajeti hiyo vilevile.

Bajeti hiyo inayozozaniwa ilitengea Idara ya Huduma za Nairobi (NMS) Sh27.1 bilioni na kuachia utawala wa Bw Sonko Sh8.4 bilioni na bunge hilo la kaunti Sh2 bilioni.

Serikali ya Kaunti ya Nairobi imekuwa ikitumia asilimia 25 ya bajeti ya kila mwaka au takriban Sh8.5 bilioni – kuendesha shughuli zake za kila siku tangu Juni. Hata hivyo, jambo hilo lilisitishwa na Mdhibiti wa Bajeti, Bi Margaret Nyakango baada ya bajeti kupitishwa.

Msemaji wa Gavana Sonko, Bw Ben Mulwa, alithibitisha kuwa serikali ya kaunti hiyo haina uwezo wa kutumia fedha kwa matumizi ya kila siku na ya kimaendeleo hadi bajeti mpya itakapoidhinishwa na kuanza kuachilia fedha za kaunti.

Hata hivyo, alisema, bajeti hiyo inayozingirwa na utata haiwezi kutekelezwa pasipo Gavana Sonko kutia sahihi idhini – nakala inayotoa kibali cha kutoa hela kutoka kwa Hazina ya Mapato ya Kaunti.