Michezo

Msimu wa ligi kuu ya Uholanzi wafutiliwa mbali

April 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSIMU huu wa 2019-10 umefutiliwa mbali katika Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie); na kwa sasa hapatakuwepo mshindi wala kikosi kitakachoshushwa ngazi.

Maamuzi hayo yanachochewa na hatua ya serikali ya Uholanzi kupiga marufuku shughuli zote za michezo nchini humo hadi Septemba 1, 2020 ili kukabiliana vilivyo na janga la virusi vya corona.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Uholanzi (KNVB), itakuwa vigumu zaidi kwa sasa kuandaa mashindano yoyote ya Eredivisie katika juhudi za kukamilisha kampeni za msimu huu.

Hadi kufutiliwa mbali kwa msimu huu mzima wa Eredivisie, Ajax walikuwa wamejizolea jumla ya alama 56 zilizowaweka kileleni mwa jedwali baada ya mechi 25.

AZ Alkmaar waliokuwa pia wamejizolea alama 56 walikuwa katika nafasi ya pili kutokana na uchache wa mabao yao. Feyenoord walikuwa katika nafasi ya tatu kwa alama 50, moja pekee kuliko PSV Eindhoven waliofunga orodha ya nne-bora katika jedwali la ligi hiyo ya vikosi 18.

Ilivyo, Ajax na Alkmaar watafuzu kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao, japo suala hilo litasubiri zaidi kurasimishwa na vinara wa mapambano hayo ya haiba kubwa.

Kwa kuwa hakuna kikosi kitakachopandishwa wala kuteremshwa daraja kwa minajili ya msimu ujao, inamaanisha kwamba kikosi cha Cambuur kilichokuwa kikijivunia pengo la alama 11 kileleni mwa Ligi ya Daraja ya Kwanza kitasalia katika kivumbi hicho mnamo 2020-2021.

Katika mahojiano yake na runinga ya NOS nchini Uholanzi, kocha Henk de John wa Cambuur alisisitiza kwamba maamuzi ya kufutilia mbali msimu huu wote wa Eredivisie ndiyo ya “kusikitisha zaidi katika historia ya soka ya taifa hilo”.

Kwa upande wao, KNVB walisema: “Ililazimu hatua fulani kuchukuliwa na matokeo ya hatua hiyo yasingemridhisha kila mtu. Kuna yule angehisi kuumizwa au hata kuonewa.”

“Itakuwa vyema iwapo washikadau wote kuanzia kwa mashabiki, wachezaji, wakurugenzi na marefa wa Eredivisie wataelewa kwamba afya ya umma siku zote ndiyo muhimu zaidi na inayostahili kuja kwanza,” ikasema sehemu ya taarifa ya shirikisho hilo.

Kufikia jana, zaidi ya watu 4,000 walikuwa wameaga dunia kutokana na virusi vya corona nchini Uholanzi.

Ni mara ya kwanza tangu 1956 kwa msimu wa Eredivisie kukamilika bila ya timu yoyote kutawazwa mshindi. Katika taarifa yake, KNVB ilishikilia kwamba isingewezekana kupandisha ngazi kikosi chochote kutoka Ligi ya Daraja ya Kwanza bila ya kushusha kingine daraja kutoka Eredivisie.

KNVB ilisema kwamba hatua yao ilikuwa zao la mashauriano ya kina kati ya wadau wote ambao pia hawakuafikiana walipopewa fursa ya kupiga kura ambayo matokeo yake yangeamua iwapo vikosi vya mwisho katika Eredivisie vingeteremshwa ngazi huku vya kwanza katika Ligi ya Daraja ya Kwanza vikipandishwa daraja.

“Wadau walipiga kura ya “hakuna kushuka daraja wala kupanda daraja” au “kuna kushuka daraja na kupanda daraja”.

Baada ya matokeo kuonyesha kwamba kila upande ulikuwa na idadi sawa ya kura, KNVB iliamua kuingilia kati na kuamua kutopandisha ngazi wala kuteremsha daraja kikosi chochote.

“Hapakuwepo na utaratibu mwafaka wa kupandisha daraja klabu zozote wala kuteremsha ngazi vikosi vyovyote kwa sababu hadi kufutiliwa mbali kwa msimu huu, kulikuwa bado na raundi nyingi za mechi za kusakatwa na washiriki kabla ya muhula kukamilika rasmi,” ikasema taarifa ya KNVB.

Feyenoord sasa watafuzu kushiriki hatua ya makundi ya Europa League msimu ujao huku PSV na Willem II wanaoshikilia nafasi za nne na tano mtawalia wakijikatia tiketi za kunogesha mchujo wa kivumbi hicho iwapo wataidhinishwa na Uefa.

Kwa upande wa wanawake, Ligi Kuu ya Eredivisie pia imekamilika bila mshindi msimu huu huku PSV wakipokezwa tiketi ya kushiriki kipute cha UEFA nao Ajax ambao wanashikilia nafasi ya pili jedwalini wakifuzu kwa mchujo muhula ujao.