Makala

Msimu wa mvua, mafuriko ndio bora kununua shamba

Na SAMMY WAWERU August 19th, 2024 2 min read

MAFURIKO yaliyoshuhudiwa maeneo tofauti ya nchi miezi kadha iliyopita, yalisababisha athari kubwa itakayochukua muda mrefu kwa waathiriwa ‘kusimama tena’.

Idadi kubwa ya watu walipoteza maisha na mali kusombwa, sehemu zilizoathirika zaidi na janga hilo zikiwa mitaa ya mabanda mijini.

Kaunti ya Nairobi, ilikuwa kati ya miji iliyogonga vichwa vya habari maafa yakiripotiwa.

Hali kadhalika, mitaa ya kifahari – inayoishi mabwanyenye, pia haikusazwa na mafuriko hayo.

Maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini kwa ushirikiano na wenzao wa Idara ya Majanga (NDMA), walijikaza ili kuokoa maisha.

Serikali ikidhihirisha wazi kutokuwa na mikakati na mipangilio kabambe kukabiliana na athari zinazoletwa na mafuriko yanaposhuhudiwa, wawekezaji wa majumba ya kibinafsi na ya kibiashara wanapaswa kukagua kwa kina ardhi wanazolenga kununua.

Msimu wa mvua ndio bora zaidi kwa shughuli hiyo.

Wakati wanapong’ang’ana kujenga na kumiliki majengo, mafuriko yawe funzo la kuwakumbusha athari ili wasijipate kwenye njia panda.

Msimu wa mvua uwe wakati mwafaka kuchambua maeneo wanayolenga kuwekeza.

Mtaro mbovu wa majitaka eneo la Zimmerman, Nairobi uliopita kati ya majengo ya kupangisha, wakati wa mafuriko ya 2024. PICHA|SAMMY WAWERU

“Mifumo na miundomsingi ya kusafirisha maji inapaswa kutiliwa maanani sana,” anasema Charles Wachira, ajenti wa kuuza mashamba.

Wachira anafanya kazi na Shirika la Prime Silver Investment Ltd.

Anatilia mkazo umuhimu wa kuelewa thamani halisi ya ardhi unayopanga kuwekeza, akipendekeza kuwepo na majadiliano na kutafuta ushauri kutoka kwa Wizara husika ya Ardhi.

“Mbali na uchunguzi wa kisheria unaofungamana na umiliki, mja pia anafaa kukagua kibinafsi hali ya mifumo ya usambazaji maji hasa mvua kubwa inaposhuhudiwa. Huu ndio wakati mwafaka wa kujinyakulia ardhi salama kuwekeza,” Wachira akaambia Taifa Dijitali kupitia mahojiano ya kipekee.

Wakati unapochagua kipande cha ardhi, kumhusisha wakili kuandaa makubaliano ya kisheria ya ununuzi ni suala muhimu.

Ben Wamalwa, ambaye ni mkulima kutoka Magharibi mwa Kenya, anasisitiza umuhimu wa kutekeleza ukaguzi wa jinsi udongo ulivyo kwenye ardhi unayopanga kumiliki.

Maji yaliyozingira nyumba za kupangisha mtaani Zimmerman, Nairobi mafuriko yaliposhuhudiwa 2024. PICHA|SAMMY WAWERU

Ripoti za majumba kusombwa na maji kutokana na hali duni ya udongo na mmomonyoko wa ardhi, aghalabu si ngeni Nairobi na maeneo yenye miinuko kama vile Murang’a na sehemu kadha Bonde la Ufa.

“Kwa mfano, udongo unaotuamisha maji (cotton soil) si bora sana katika shughuli za kilimo. Isitoshe, hakikisha unachunguza kwa kina maeneo yenye miinuko kabla ya kununua shamba,” anashauri Wamalwa.

Wamalwa ni mkulima hodari na mwekezaji kwenye majumba ya kupangisha.

Aidha, anapendekeza uchimbaji mitaro, upanzi wa nyasi za mifugo kama vile za mabingobingo (Napier grass) ili kudhibiti kasi ya maji yanayotiririka.

Mafuriko yaliyoshuhudiwa, yalifichua utepetevu uliopo katika kuboresha miundomsingi ya maji na vivukio – madaraja kwenye mito na barabara.

Licha ya tahadhari kutolewa na idara ya hali ya anga na zile husika, serikali bado inaonekana kulegea maeneo yaliyoathirika yakisalia yalivyokuwa.

Imetafsiriwa na Kalume Kazungu