NA CHARLES WASONGA
IDARA ya Utabiri wa Hali ya Anga imetangaza kuwa msimu wa mvua nyingi unaosubiriwa kwa hamu utaanza wikendi hii katika maeneo kadha ya nchi.
Msimu huo wa mvua ya masika huanza mwezi Machi hadi Mei kila mwaka katika maeneo ya Magharibi, Nyanza, Bonde la Ufa na Kati mwa Kenya ambako wakulima huitegemea kwa upanzi wa mimea ya chakula.
Kulingana na utabiri wa hivi punde wa Idara hiyo mvua nyepesi inatarajiwa kushuhudiwa katika kaunti za Siaya, Kisumu, Homa Bay Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Nandi, Laikipia, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega na Bungoma wikendi hii na juma lijalo.
Mvua nyingi pia zinatarajiwa kushuhudiwa katika maeneo kadha ya kaunti za Nairobi, Nyandarua, Nyeri, Meru, Embu, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu na Tharaka Nithi.
“Kwa hivyo, wakulima katika maeneo yatakayopokea mvua wanashauri kushirikiana na maafisa wa Wizara ya Kilimo ili kupata maagiza kuhusu mbegu bora za kupanda pamoja na mbinu bora za kilimo za kukumbatia ili kupata mavuna bora,” ikasema taarifa hiyo.
Kulingana na utabiri huo, sehemu chache katika ukanda wa Kaskazini Mashariki unaojumuisha kaunti za Garissa, Wajir, Mandera, Isiolo na Marsabit pia zitapata mvua nyepesi kuanzia Jumatatu, Machi 12, 2023.
Hata hivyo, Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga inatabiri kwamba maeneo ya Kajiado Kusini na kaunti za Makueni, Machakos, Taita Taveta, Kitui zitasalia kavu bila mvua kuanzia Jumatatu hadi mwishoni mwa mwezi huu.
Kaunti za Pwani kama vile; Mombasa, Tana River, Lamu, Kilifi na Kwale zitaanza kushuhudia mvua nyingi mwanzoni mwa Aprili.