Michezo

Msimu wa raga Kenya kufutwa mechi zisipokamilika

June 4th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KLABU za raga zinazoshiriki Ligi Kuu ya Kenya Cup zimetaka kampeni za msimu huu wa 2019-20 kutamatika rasmi kufikia Oktoba 2020.

Xavier Makuba ambaye ni mwenyekiti wa Kenya Cup, amesema huenda wakalazimika kufutilia mbali msimu huu mzima wa raga iwapo mechi zilizosalia katika kivumbi hicho hazitakuwa zimesakatwa kufikia wakati huo.

“Oktoba ndio mwezi wa mwisho ambao klabu zimeafikiana kukamilisha kampeni za raga msimu huu. Nadhani kuna muda wa kutosha kufanikisha maandalizi ya michuano yote kabla ya kipindi hicho,” akasema Makuba.

“Tungali na Juni, Julai, Agosti na Septemba yote kujiandaa kwa mechi za Kenya Cup na kampeni za Sevens ambazo zitasakatwa pia katika kipindi hicho. Huu ni muda wa kutosha,” akasema Makuba ambaye pia ni mwenyekiti wa kikosi cha wanabenki wa KCB.

Mojawapo ya mapendekezo ambayo pia yametolewa na vikosi vya Kenya Cup ni kufutilia mbali kivumbi cha Enterprise Cup ili kufanikisha mipango ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu muhula huu.

Hadi kusitishwa kwa shughuli zote za michezo humu nchini mnamo Machi 2020, pambano la Enterprise Cup ambalo ndilo kongwe zaidi katika historia ya raga ya Kenya, lilikuwa limetinga hatua ya nusu-fainali.

Kabras Sugar ambao ni mabingwa watetezi walikuwa wamepangwa kuvaana na Homeboyz huku wanabenki wa KCB wakimenyana na Impala Saracens.

Katika Kenya Cup, Homeboyz wanatarajiwa kuchuana na Menengai Oilers ambapo mshindi atajikatia tiketi ya kukabiliana na mabingwa watetezi, KCB katika hatua ya nusu-fainali ya Kenya Cup.

Kabras watapimana ubabe na mshindi kati ya Impala na Mwamba RFC. Hadi kipute cha Kenya Cup kilipofutiliwa mbali muhula huu, Kabras RFC walikuwa ikiselelea kileleni kwa alama 74, tatu zaidi mbele ya KCB.