Msimu wa talaka

Msimu wa talaka

Na LEONARD ONYANGO

HUKU ikiwa imesalia miezi 12 kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, wanasiasa wameanza kujipanga kwa kutalikiana na washirika wao wa sasa ili kuzidisha nafasi yao ya kushinda viti mwaka 2022.

Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka tayari ametangaza talaka mbili dhidi ya Kinara wa ODM Raila Odinga na Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana.

Chama cha Wiper, Jumatatu, kilitangaza kujiondoa NASA huku kikisema kuwa, kimefungua milango ya mazungumzo na vyama vingine kwa lengo la kuunda serikali ijayo.

Muungano wa NASA uliobuniwa Februari 2017, ulijumuisha Bw Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford Kenya), Bw Musyoka na Isaac Ruto (Chama cha Mashinani).

Mkutano wa Kamati Kuu (NEC) wa ODM, Alhamisi, uliidhinisha chama hicho kujiondoa NASA.

Kulingana na duru ndani ya ODM, Bw Odinga aliamua kujiondoa NASA kumaliza presha kutoka kwa Mabw Mudavadi na Musyoka ambao wamekuwa wakisisitiza kuwa waziri mkuu huyo wa zamani ni sharti arudishe mkono kwa kuunga mkono mmoja wao 2022.

Chama cha ANC, wiki mbili zilizopita, kilisema kuwa, kimemwandikia barua Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu kutaka kujiondoa NASA.

Lakini Bi Nderitu, jana alisema kuwa hajapokea barua ya chama chochote kikitaka kujiondoa NASA.

“Sijapata barua kutoka kwa chama chochote. Labda bado wanaandika,” Bi Nderitu aliambia Taifa Leo.

Kulingana na mkataba wa maelewano, muungano wa NASA utavunjwa iwapo vyama vitatu vitajiondoa.

“Kufikia sasa, muungano wa NASA ungalipo kwani hakuna chama ambacho kimejitoa rasmi,” akasema Bi Nderitu.

Mabw Odinga, Mudavadi, Musyoka na Wetang’ula wamekuwa pamoja tangu 2012 licha ya kutalakiana mara kwa mara.

Mnamo 2012, viongozi hao waliunda muungano wa Coalition for Reforms and Democracy (Cord). Miaka mitatu baadaye, ODM ilijiondoa CORD.

Lakini mnamo 2017, wanne hao walikuja pamoja tena na kuunda NASA ambapo Bw Odinga alipeperusha bendera ya muungano.

Afisa wa ngazi ya juu ndani ya ODM, aliambia Taifa Leo kuwa, Bw Odinga sasa anashirikiana na Rais Uhuru Kenyatta kushawishi Mabw Mudavadi, Musyoka, Wetang’ula na kiongozi wa Kanu Gideon Moi kuunda muungano utakaogeuka wimbi kali la kisiasa litakalozuia Naibu wa Rais William Ruto kuingia Ikulu mwaka ujao.

Jumatatu, Bw Musyoka alisema kuwa chama chake kimesalia ndani ya miungano na Jubilee pamoja na Kenya One Alliance (OKA).

Hiyo inamaanisha kuwa Bw Musyoka ametamatisha miungano baina ya Wiper na Muungano Party chake Prof Kibwana pamoja na muungano na Uzalendo chake Bi Wavinya Ndeti.

Kanu, hata hivyo, imeonyesha dalili za kutaka kutoroka muungano wa OKA ambao haujasajiliwa rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat, chama hicho hakiko tayari kutia saini mkataba na vyama vilivyo katika OKA.

“Chama cha Kanu kilifanya muungano na Jubilee na hatujajitoa. Tutaunga mkono Rais Kenyatta hadi mwisho wa muhula wake wa pili ndipo tufikirie kujiunga na muungano mwingine,” akasema Bw Salat.

Bw Moi anaoenekana kuegemea upande wa Bw Odinga huku Bw Mudavadi na Bw Musyoka wakisisitiza kuwa ni sharti wawe debeni 2022.

Naye, Gavana wa Pokot Magharibi John Lonyangapuo ambaye ni gavana wa pekee wa Kanu, ametangaza kugura chama hicho na badala yake ataunda chama atakachotumia kutetea kiti chake.

Gavana wa Kilifi Amason Kingi amekuwa akimkwepa Bw Odinga kila anapozuru eneo la Pwani – hatua ambayo imefasiriwa kuwa amegura ODM.

Bw Kingi amekosa kuhudhuria mikutano ya Bw Odinga mara kadhaa na kuzua minong’ono kwamba huenda anaelekea kwa Dkt Ruto.

Naibu wa Rais alitalikiana kisiasa na Rais Kenyatta miezi michache baada ya uchaguzi wa 2017 na kuna uwezekano finyu kwamba atamuunga mkono kwenye kinyang’anyiro cha urais 2022.

Ushindi wa United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Dkt Ruto, katika uchaguzi mdogo wa Kiambaa, Kaunti ya Kiambu, umetia hofu wandani wa Rais Kenyatta katika eneo la Mlima Kenya.

Baadhi ya viongozi wa Jubilee wanasema kuwa uhusiano wa karibu kati ya chama hicho tawala na ODM, ulisababisha mwaniaji wao Kariri Njama kupoteza.

You can share this post!

Mlipuko Beirut mwaka 2020 wasababishia raia umaskini

Wanasiasa wakuu watatii kanuni au wataendelea kupepeta...