Michezo

Msimu wote wa raga wafutiliwa mbali nchini

April 11th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) limefutilia mbali msimu mzima wa 2019-20 kutokana na janga la virusi vya homa kali ya corona.

Haya ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa KRU, Ian Mugambi ambaye amekiri kuwa mlipuko wa corona umelemaza kabisa ulingo wa raga na michezo yote ya humu nchini.

KRU linakuwa shirikisho la kwanza la michezo nchini Kenya kufutilia mbali msimu mzima kwa hofu ya maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

Hatua ya KRU inaathiri Ligi Kuu ya Kenya Cup, KRU Championship, ligi pana za kitaifa, ligi za madaraja ya chini, Enterprise Cup, Great Rift Valley Cup, Mwamba Cup na ligi ya kitaifa ya National Cirucit.

“Kufutiliwa mbali kwa kipute chote cha msimu huu kunamaanisha kwamba hakuna kikosi kitakachopandishwa ngazi wala kuteremshwa daraja. Vikosi vyote vinasalia katika ligi zilizokuwa zikishiriki muhula huu na hakuna mshindi wa kipute chochote kati ya vyote ambavyo vimetandazwa kufikia sasa,” akasema Mugambi kwa kukariri kwamba KRU itafichua hivi karibuni ratiba ya kujifua kwa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande, Shujaa, kwa minajili ya duru zilizosalia katika kampeni za Raga ya Dunia msimu huu.

Hii ni baada ya kuahirishwa pia kwa duru za London na Paris hadi Septemba kutokana na corona.

Kwa mujibu wa Thomas Odundo ambaye ni mkurugenzi wa raga wa KRU, vinara wa shirikisho na wadau wote husika katika kikosi cha Shujaa wamekuwa wakishauriana na watatoa mwelekeo utakaokumbatiwa na timu ya taifa chini ya mkufunzi mzawa wa New Zealand, Paul Feeney.

Kufikia sasa, Shujaa wanashikilia nafasi ya 11 kwa alama 35 kwenye msimamo wa jedwali baada ya kunogesha duru sita za Raga ya Dunia msimu huu wa 2019-20.

Vipute vya Kenya Cup na KRU Championships vilikuwa viingie hatua ya mchujo mnamo Machi 14 huku nusu-fainali zikiandaliwa Machi 21, wiki mbili kabla ya fainali.

Nusu-fainali za Enterprise Cup zilikuwa zifanyike mnamo machi 28 na fainali kupigwa Aprili 18, 2020.

Hadi kufutiliwa mbali kwa Ligi Kuu ya Kenya Cup, Kabras Sugar walikuwa wakiselelea kileleni kwa alama 74, tatu zaidi mbele ya mabingwa watetezi, KCB.

Homeboyz walikuwa wakutane na Menengai Oilers katika mchujo na mshindi akijikatia tiketi ya kuvaana na KCB katika nusu-fainali ya kwanza. Mshindi kati ya Impala Saracens na Mwamba angalikutana na Kabras katika nusu-fainali nyingine.

Kwa upande wa KRU Championship, Strathmore Leos waliokuwa hawajapoteza mechi yoyote, walikuwa wakiongoza jedwali kwa alama 76, tisa zaidi kuliko Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) katika nafasi ya pili.

Leos walikuwa wakutane na mshindi kati ya Northern Suburbs na Chuo Kikuu cha USIU-A katika mojawapo ya nusu-fainali huku MMUST wakipimana ubabe na mshindi kati ya Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi na Egerton Wasps.

Mnamo Machi 13, serikali ilipiga marufuku shughuli zote za michezo baada ya kisa cha kwanza cha corona kuthibitishwa humu nchini. Pindi baadaye, mapambano ya Great Rift Valley kwa wachezaji 10 kila upande yaliyokuwa yaandaliwe kati ya Aprili 10-13, 2020 yalisitishwa.

Kipute hicho cha siku tatu kilichokuwa kilete pamoja wanaraga wa haiba kubwa kutoka Ligi Kuu ya Kenya Cup na ligi nyinginezo za madaraja ya chini kote nchini sasa kitaandaliwa Aprili 2021.

Menengai Oilers walitawazwa mabingwa wa makala ya Great Rift Valley mjini Nakuru mwaka jana baada ya kuwapepeta mabingwa wa 2018, Homeboyz 10-5 katika fainali.