Makala

Msingi wa Mlima Kenya kumkaidi Uhuru watolewa ufafanuzi

June 19th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

MATUMAINI ya wanaolenga kutwaa kura za Mlima Kenya kupitia ushawishi wa Rais Uhuru Kenyatta eneo hilo wanaonywa kuwa huenda waangukie pua kufuatia kudorora kwa umaarufu wake miongoni mwa wenyeji.

Sio siri kuwa kuna ukaidi mkuu kwa Rais ambapo umemwingia hadi kwa bongo lake na kwa hasira, amejitokeza hadharani kuteta kuwa atalipiza kisasi kupitia kung’atua mamlakani wanaofadhili ukaidi huo.

Kwa sasa, kuna minong’ono ya wazi kuwa sera zake za kiutawala pamoja na kutotimiza ahadi zake za kampeni za 2017 kwa wenyeji kumechangia pakubwa taswira kuwa aliwahadaa.

Gharama ya maisha kupanda pamoja na mfumkobei, kuonekana wazi kukosa kutoa mwongozo wa kisiasa na pia kukaa kimya wakati sera zinatekelezwa ambazo zinaathiri pakubwa kiuchumi wazawa wa eneo hilo ni miongoni mwa sababu ambazo zinatolewa.

Katika mijadala ya kisiasa mitaani, kuna taswira ya maafikiano kuwa utawala wake ulikuwa makosa makuu yaliyoidhinishwa na wenyeji kupitia kumpigia kura.

Ni taswira ambayo inaelezewa hata na viongozi wa eneo hilo, japo kwa njia isiyo ya kujianika kama wakaidi kwa ‘serikali ya nyumbani’ na ambapo mafumbo yanatandazwa ya kuonyesha kuwa “mtu wetu ametusaliti.”

Katika mitandao ya kijamii, kauli mbiu ya kuwatokeza wenyeji kupigia Rais Kenyatta kura ya “Thuraku Kumira Kumira” ikiwa na maana “Siafu wajitokeze kwa asilimia 100” imeanza kukejeliwa ikitajwa kama kauli ya hadaa inayotesa kwa sasa na iliyoishia kuwa sawa na ujinga wa maamuzi.

Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu anakubali kuwa kuna shida kubwa kwa sasa na imani ya wenyeji kwa ‘serikali yao’ imeishiwa na imani.

“Hii sera ya kubomolea wafanyabiashara vioski vyao bila kuwapa mahala mbadala pa kujitafutia riziki imepunguzia serikali umaarufu. Ni sera ambayo inaonekana kusukumwa kimakusudi na Gavana wa Nairobi, Mike Sonko ili kuzua ukaidi miongoni mwa wenyeji Mlima Kenya,” anasema Waititu.

Kuzima umaarufu

Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri anateta kuwa kuna taswira ya Rais Kenyatta kuanza kutekwa nyara na mirengo ya kumharibia umaarufu ili asiwe na uwezo wa kutoa mwongozo mwafaka wa 2022 na iishie Mlima Kenya kutengwa.

Anasema kuwa kuna hatari kubwa sana kwa kuwa Rais Kenyatta haonekani kung’amua hilo na badala yake amebakia kimya huku eneo hilo likiwa limezama katika imani kuwa awamu yake ya pili na ya mwisho ikulu ilikuwa iwape kipaumbele katika kuwaboreshea maisha.

Aliyekuwa mbunge wa Naivasha, John Mututho tayari amejitokeza waziwazi akisema kuwa “kwa sasa hakuna haja ya kujidanganya kuwa Rais ana ule ushawishi wa kuelekeza wenyeji kumuunga mkono yeyote.”

Anasema kuwa Rais amejikwaa pakubwa katika sera yake ya uongozi ya kuongeza ushuru na kupanda kwa deni la kitaifa, hali ambazo zimechangia gharama ya kufanya biashara miongoni mwa wawekezaji wa eneo hilo kukumbwa na kudorora kwa faida.

Aliyekuwa mwenyekiti wa wawaniaji wa Jubilee Mlima Kenya 2017, Samuel Maina ameonya kuwa Rais alifika ikulu na akasahau jinsi wenyeji walijituma Agosti 8, 2017, kumrejesha Ikulu na pia katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.

“Yeye mwenyewe (Rais) alizunguka eneo hili akituonya kuwa utawala wake ulikuwa katika hatari ya kung’atuliwa na Raila Odinga. Wenyeji wakajitokeza kwa wingi wao wakiwa na kura mkononi kumpigia na akafanikiwa kujiepushia balaa ya kuondolewa afisini. Tukaamrishwa na Jaji David Maraga na majaji wenzake katika mahakama ya juu zaidi turudie kura hiyo na tukafanya vivyo hivyo na tukahifadhi uongozi wake Ikulu,” anasema Mututho.

Anasema kuwa baada ya kuapishwa kuwa Rais, alikumbatia Odinga ndani ya serikali na akaibua hali ya Wakenya kuumizwa na sera mbovu za uongozi bila ya kuwa na mtetezi kwa kuwa upinzani ni kama vile uliaga dunia na kuzikwa katika kaburi la sahau katika utawala huu wa sasa.

“Leo hii, tukiibiwa kiuchumi na mafisadi, hakuna wa kututetea. Serikali ikikopa kiholela na kupandisha ushuru kwa njia za kikatili, hakuna wa kututetea. Ni kama Rais alimwendea Odinga waridhiane ndio Wakenya waumizwe kisawasawa,” anasema.

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu, William Kabogo anesema kuwa utawala wa Rais Kenyatta kwa sasa umeingiwa na hatari kuu ya kukaidiwa.

Anasema kuwa kwa sasa kuna wingu la ukaidi ambalo linajichora Mlima Kenya na ambalo linafaa kushughulikiwa.

Na katika hali hiyo, Rais Kenyatta anaonekana waziwazi eneo hilo kama aliyesaliti matumaini kwa ahadi zake kuwa angetumia awamu yake ya pili mamlakani kuwatuza wenyeji Mlima Kenya mgao wao wa haki wa hisa za serikali yake iking’amuliwa kisiasa kuwa kura za eneo hilo kwa kiwango kikuu zilinusuru meli yake ya uwaniaji kutozamishwa na upinzani.