Michezo

MSINILAUMU: Mourinho asema hafai kulaumiwa kwa matatizo Spurs

February 12th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Jose Mourinho amesema hafai kulaumiwa kwa matatizo yanayokumba klabu ya Tottenham Hotspur.

Raia huyo wa Ureno amejitetea kwamba amelazimika kutumia wachezaji katika nafasi ambazo si zao.

Kutokuwepo kwa nahodha Harry Kane kumemwacha kocha huyo bila mshambulizi wa kutegemea. Son Heung-min si mshambuliaji wa katikati, lakini inabidi acheze katika nafasi hiyo.

Kadhalika, Lucas Moura si mshambuliaji wa kutegemea katika nafasi hiyo, lakini inabidi acheze hapo.

Matatizo kama hayo yanavuruga mipango ya kocha huyo katika safu ya ulinzi ambako inabidi Ryan Sessegnon acheze kama beki wa kushoto, nafasi isiyokuwa yake.

Isitoshe, Mourinho amedai kwamba baadhi ya wachezaji hawajaanza kuelewa majukumu yao kikamilifu pale kikosini.

Kuna majeraha kwa wachezaji wake tegemeo, lakini inabidi aunde timu ya kucheza, huku akidai kwamba ni makocha wachache wanaoweza kukubali hali ngumu kama hiyo.

“Hali hii naifananisha na mtu ambaye amejifunika blanketi, huku miguu yake ikiwa nje.”

Kocha huyo aliwahi kutoa madai kama hayo majuzi baada ya Spurs kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Southampton katika mechi ya marudiano ya Kombe la FA.

“Kikosi chetu kiko katika hali kama hiyo ya kujifunika blanketi huku miguu ikiwa nje, lakini kwa jumla kila mtu anapigana vikali, licha ya hali hiyo ya kushangaza.”

“Nimepitia katika hali hii hapo awali. Wakati mmoja tunakuwa na wachezaji A, B, C nje halafu katika mechi inayofuata tunakuwa na D, E na F.”

Tayari bila Kane, Ben Davies na Moussa Sissoko, inabidi kocha huyo awape nafasi wachezaji wa akiba Giovani Lo na Erik Lamela waliokuwa na majeraha, huku akiongeza kwamba Dele Alli ni mzuri anapoingia mechi ikiendelea.

“Hata dhidi ya Manchester City, nisingeweza kucheza mfumo wangu wa 4-3-3 kwa sababu sikuwa na wachezaji wa kutosha kuucheza, ingawa tulishinda kwa 2-0.”

Ilibidi Mourinho atumie mfumo wa 3-5-2, huku akiwaanzisha Son na Lucas kama washambuliaji wa katikati, wakati Ndomele ambaye ni mshambuliaji akicheza na mtu wa kusambazia washambuliaji mipira.

“Tumeshindwa kucheza vizuri kwa sababu baadhi ya wachezaji wameshindwa kucheza vizuri kwa dakika zote 90, na itakuwa vigumu zaidi iwapo mechi itaenda katika muda wa ziada,” Mourinho alisema.

“Timu inapaswa kuwa na kikosi kamili, pamoja na wachezaji wa akiba ambao wanaongeza moto wanapoingizwa uwanjani. Mechi inapokuwa ngumu, timu inahitaji watu kama Dele Alli, Lamela na Lo Celso kuingia,” aliongeza.