Habari Mseto

Msinisikitikie, Sonko aambia wakazi wa Nairobi

September 21st, 2019 1 min read

Na FATUMA BUGU

GAVANA wa Nairobi, Mike Sonko, amewaambia viongozi na wakazi wa Nairobi wasimsikitikie kufuatia misukosuko inayomkumba.

Bw Sonko aliwaomba viongozi wa Nairobi waendelee kufanya maendeleo ya kuboresha jiji na waache maafisa wa upelelezi wafanye kazi yao.

“Shida yangu ni shida yangu kama Sonko, si shida ya wakazi wala maendeleo ya Nairobi, kwa hivyo shida yangu mniachie,” alisema Bw Sonko.

Bw Sonko alisema kuwa anamuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji pamoja na maafisa wa upelelezi katika kuangamiza ufisadi nchini.

“Hii ni hali yangu, nyinyi muendelee na muungane mikono kama wakazi wa Nairobi, mimi sitaongea kitu kwa sasa hadi uchunguzi ukamilike,” alisema Bw Sonko.

Pia, alipinga madai kuwa alijificha na kudai kuwa yeye hatishwi na chochote.