Habari Mseto

Msipokujia pikipiki, tuktuk na simu zenu tutazipiga mnada, polisi watangazia umma

February 5th, 2024 1 min read

NA WINNIE ATIENO

MAAFISA wa polisi katika Kaunti za Mombasa na Kilifi wanatarajia kupiga mnada zaidi ya pikipiki na tuktuk 50 endapo wamiliki hawataenda kuzichukua.

Kwa mujibu wa notisi kwenye gazeti rasmi la serikali, Mahakama ya Hakimu Mwandamizi Mkuu eneo la Mariakani aliagiza wamiliki wa tuktuk na pikipiki hizo zilizo katika kituo cha polisi cha Rabai kuenda kuzichukua la sivyo zitapigwa mnada.

Wamiliki hao wamepewa siku saba kuanzia Ijumaa iliyopita kuzichukua, la sivyo au zitapigwa mnada.

Katika Kaunti ya Mombasa, pikipiki hizo na tuktuk ziko katika kituo cha polisi cha Bamburi.

Mali nyingine ambazo zimeorodheshwa kwa mnada katika kituo cha Bamburi ni simu 19 za rununu, runinga, mbao, madirisha, miongoni mwa mengine.

Ingawa ilani hizo hazijaeleza mali hizo zilikotoka, inaaminika baadhi zilinaswa kutoka kwa washukiwa wa wizi, makosa ya trafiki, au katika mizozo ya umiliki.

Mnada mwingine umepangiwa kufanywa pia na kituo cha polisi cha Maua, Kaunti ya Meru.

Kampuni ya upigaji mnada ya Autoland Auctioneers ndio imepangiwa kusimamia mnada wa mali ambazo zitakuwa hazijachukuliwa na wamiliki wao katika muda ulioekwa.