Msipounga Raila mtajuta, ODM yaambia OKA

Msipounga Raila mtajuta, ODM yaambia OKA

Na SHABAN MAKOKHA

VIONGOZI wa ODM, wamepuuza azma ya urais ya muungano wa One Kenya Alliance (OKA) wakisema vinara wake watajuta wakikosa kuunga aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

Naibu kiongozi wa ODM, Wycliffe Oparanya, amewataka vinara wa OKA watupilie mbali azma yao ya kuwania Urais na badala yake wamuunge mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Oparanya ambaye ni Naibu Kiongozi wa ODM amewataka Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Gideon Moi (KANU) na Moses Wetang’ula wabadili uamuzi wao wa kuwania kiti hicho na badala yake washirikiane na Bw Odinga.

Gavana huyo anayehudumu kipindi cha pili aliahidi kuwa Bw Odinga ataongoza tu kwa muhula mmoja kisha kumwachia mwanasiasa mwengine akibashiri kuwa mmoja wa viongozi kutoka eneo la Magharibi atarithi kiti hicho kutoka kwake 2027.

Mabw Musyoka, Mudavadi na Wetang’ula walikuwa washirika wa Bw Odinga katika uliokuwa muungano wa NASA kabla ya kutofautiana wakimlaumu Bw Odinga kwa kukosa kutii makubaliano waliyokuwa nayo kwenye uchaguzi wa 2017.

Hata hivyo, Bw Oparanya amesema watatu hao ndio watapoteza zaidi kwa kuwa tayari ushindani wa kiti cha urais umechukua mkondo wake na ni kati ya Bw Odinga na Naibu Rais Dkt William Ruto.

“Kwa sasa Mudavadi hawezi kuvutia kura za kutosha kumwezesha kushinda kiti cha urais. Anafaa amuunge mkono Raila Odinga ambaye ameahidi kwamba ataongoza kwa muhula mmoja pekee kisha mmoja kutoka jamii ya Waluhya atarithi kiti hicho,” akasema Bw Oparanya ambaye alikuwa akizungumza katika eneobunge la Lugari.

Gavana huyo ambaye pia aliwahi kuhudumu kama mbunge wa Butere, alisema Bw Odinga yupo pazuri sana kutwaa uongozi wa nchi na anafaa zaidi kwa kuwa ni kiongozi ambaye anaelewa matatizo ya kihistoria na kisiasa yanayokumba nchi hii.

Licha ya rai ya naibu huyo wa kiongozi wa ODM, Bw Mudavadi ameshikilia kuwa liwalo na liwe atakuwa debeni na ni wakati ambapo Bw Odinga anafaa kumuunga mkono mwaniaji wa Urais kutoka Magharibi kwa sababu wakazi wa eneo hilo wamempigia kura kwa miaka mingi.

Bw Mudavadi alisema hana imani tena na Bw Odinga kutokana na kile alichodai kuwa aliwasaliti vinara wenzake ndani ya Nasa kisha akaingia serikalini.

“Mara hii niko debeni hadi kura ipigwe. Kama Raila Odinga hawezi kukubali kumuunga mkono mwaniaji mwengine wa kiti cha Urais, basi tukutane kwa debe na Wakenya waamue,” akasema Bw Mudavadi.

Kauli yake iliungwa mkono na mbunge wa Lugari Ayub Savula aliyewataka Wakenya wasimpigie kura Bw Odinga au Naibu Rais akisema wawili hao wana hasira na nia ya kulipizana kisasi.

Bw Savula pia alidai kuwa umaarufu wa ODM unaendelea kupungua katika maeneo mbalimbali ya nchi.

“Hapa Magharibi ANC imefifisha umaarufu wa ODM. Pwani mwa Kenya vyama vidogo vidogo vinachipuka na kuhatarisha zaidi ubabe wa ODM. Hakuna ukweli wowote kwenye matamshi ya Oparanya kuwa Raila na Ruto ndio wapo kifua mbele kunyakua kiti cha urais. Wawili hao wamejawa na hasira na wanalenga kisasi,” akasema Bw Savula.

Iwapo Bw Odinga atawania urais, basi atakuwa akijaribu bahati yake kwa mara ya tano baada ya kukikosa kiti hicho 1997, 2007, 2013 na 2017.

Naye hii itakuwa mara ya pili kwa Be Mudavadi kugombea kiti hicho baada ya kukiwania mara ya kwanza mnamo 2013 kupitia UDF ambayo haipo tena.

You can share this post!

Are You Able To Be Completamente Genuine Within Online...

Waiguru apata marafiki wapya baada ya kukumbatia Naibu Rais