Msipoungana msahau urais milele, Ngilu aambia vinara wa Nasa

Msipoungana msahau urais milele, Ngilu aambia vinara wa Nasa

Na BENSON MATHEKA

GAVANA wa Kitui, Bi Charity Ngilu anasisitiza kuwa vinara wa NASA wasipoungana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022, wasahau urais milele.

Bi Ngilu alirudia kauli aliyotoa katika mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Kibwezi Kalembe Ndile kwamba ni kwa vinara hao -Raila Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), na Moses Wetangula (Ford-Kenya)- kuungana wataweza kumshinda Naibu Rais William Ruto.

“Wasipoungana, watakuwa wakiiona Ikulu kwenye viusasa,” alisema Bi Ngilu.

Kauli yake ilijiri siku moja baada ya Bw Musyoka kuapa kwamba hatamuunga Bw Odinga kugombea urais kwa mara ya tatu na badala yake atagombea.

Bi Ngilu alisema kwamba iwapo wanne hao kila mmoja atagombea urais kivyake, hawatatimiza ndoto zao za kuwa kwenye serikali.

“2017 tulikuwa NASA na kina Raila, Kalonzo, Musalia, Wetangulana tulikuwa tunasema kuna vitu tunataka kufanyia Kenya yetu. Hiyo, kwa sababu Jubilee iliingia, haikufanyika. Na pia tulipata handsheki, na wote wanne waliingia kwa hiyo handsheki wakasema ‘tuko na wewe Uhuru Kenyatta,’” Bi Ngilu alisema akizungumza katika kipindi cha Jambo Kenya kwenye redio citizen Alhamisi.

“Sasa badala ya kusema hatukupata 2017 tunataka ukuje na sisi tufanye ile ajenda tulikuwa nayo, kila mmoja anaongea lugha yake. Niliwaambiwa kila mmoja pekee yenu atashindwa pekee yake, kwa hivyo ni vizuri washikane pamoja vile walikuwa ili tuunde serikali. Lakini mkikosa kuungana,, kila mmoja wenu ataenda nje na atakuwa akiona hiyo nyumba ya ikulu kwa ViuSasa. Huo ndio ukweli,” alisema.

Gavana Ngilu alisema kwamba wakiungana nyuma ya mmoja wao watashinda urais kwa urahisi sana.

“Wakija pamoja, na naona sasa Gideon Moi pia ako nao, saa mbili na nusu watapeleka wale wengine nyumbani, lakini wakikosa, ni hao watapelekwa nyumbani,” alisema.

Bw Mudavadi pia amepuuza uwezekano wa kumuunga Bw Odinga kugombea urais kwa mara ya tatu akidai chama cha ODM kilisambaratisha NASA kwa kudharau washirika wake katika muungano huo.

Kauli za wawili hao zilichangamkiwa na washirika wa Dkt Ruto wakisema Bw Odinga ametorokwa na vigogo wengine wa kisiasa. Kulingana na wandani wa Dkt Ruto, Bw Odinga ndiye mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi wa urais wa 2022.

You can share this post!

Pwani kuwa na madereva 4 Safari Rally

‘Hakuna kifo cha corona jana Jumatano’