Habari Mseto

Msitarajie mvua Aprili na Mei – Idara

April 16th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

NI rasmi kwamba mvua haitashuhudiwa nchini katika msimu huu kama ilivyokuwa kawaida miaka ya nyuma, kulingana na Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga.

Kaimu naibu mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Nchini Benard Chanzu Jumanne alisema Wakenya wasitarajie mvua katika miezi ya Aprili na Mei.

Aliwataka Wakenya kuwa tayari kwa kukabiliana na changamoto za ukosefu wa maji ya kunywa, ya matumizi katika viwanda na ya kutumika katika uzalishaji wa umeme.

Bw Chanzu alisema hali hii inachangiwa na mabadiliko ya hali ya anga.

“Hakuna dalili ya mvua kunyesha wiki na dalili zinaonyesha kuwa hali hii itaendelea kushuhudiwa katika msimu huu wote. Hii ina maana kuwa mvua haitanyesha katika mwezi ujao wa Mei,” akasema, kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Ukosefu wa mvua pi umekuwa ikiandamana na kupanda kwa joto saa za mchana na usiku na kufikia sentigredi 41 katika baadhi ya sehemu haswa kaskazini mwa Kenyatta.

Hata hivyo, idara ya hali ya hewa ilisema kuwa nyanda za juu za Magharibi mwa nchini kama vile; Kisii, Nyamira, Bungoma, Trans Nzoia, Kakamega, Busia, Homa Bay na Kericho yalirekodi kiwango fulani cha mvua.

Maeneo fulani katika eneo la Kati kama vile Kiambu, Meru na Nairobi pia yanashuhudia mvua chache.

Watabiri wa hali ya anga wanasema kuwa ukosefu wa mvua nchini umesababishwa na kimbung Idai ambacho kiliathiri Musumbiji mwezi jana na hivyo kuchelewesha safari za hewa yenye uwezo wa kusababisha mvua kuja katika anga ya Kenya.