Habari Mseto

Msitarajie nyongeza ya mshahara, serikali haina hela – Uhuru

February 20th, 2019 1 min read

RUTH MBULA Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alisisitiza kuwa serikali haina pesa za kuwalipa wauguzi wanaogoma.

Akiongea akiwa Kaunti ya Kisii alipofungua hospitali mpya ya rufaa na mafunzo iliyojengwa na serikali ya kaunti hiyo, Rais Kenyatta aliwaonya wafanyakazi wa serikali dhidi ya kususia kazi kila wakati kwa ajili ya kushinikiza waongezewe mshahara.

“Wafanyakazi wetu wanafaa kufahamu kwamba hatuwezi kuwa tukijadili mambo ya mishahara kila wakati. Pesa haitoshi na hakuna wakati ambao itatosha. Wanadhani hizo pesa hutoka wapi?” alisema Rais Kenyatta.

Wauguzi katika kaunti 18 wamekuwa wakigoma kwa wiki ya tatu sasa, wakitaka serikali iwaongeze marupurupu waliyokubaliana.

Kupitia chama chao chao, wauguzi hao wamekuwa wakiteta kwamba serikali ilipuuza makubaliano.

Walikaidi agizo la mahakama kwamba warejee kazini na kushiriki mazungumzo na serikali kutatua mzozo huo.

Wiki jana, Rais Kenyatta aliagiza serikali za kaunti, ambako wauguzi wanagoma, na Wizara ya Afya kuwafuta kazi iwapo watakosa kurudi kazini. Hata hivyo, wahudumu hao wa afya walipuuza agizo hilo wakisema Rais hana mamlaka ya kuingilia masuala ya afya kwa sababu sekta hiyo imegatuliwa.

“Rais ashughulike na masuala ya usalama wa taifa na ulinzi. Aache kuingilia masuala ya wauguzi kwa sababu tuko chini ya serikali za kaunti,” alisema Katibu Mkuu wa chama cha wauguzi, Seth Panyako.

Mbali na wauguzi, walimu pia wametisha kugoma wakitaka waongezewe mishahara walivyokubaliana na serikali.

Hata hivyo, Rais Kenyatta aliwaambia kuwa uchumi wa nchi hauwezi kuruhusu mfanyakazi yeyote wa serikali kuongezewa mshahara.

“Tunapaswa kuhudumia wananchi kwanza kwa sababu tunawajibika kwao. Ikiwa kila wakati wabunge, walimu, wauguzi na wengine watakuwa wakigoma, mwananchi atatoa huduma wapi?” akauliza Rais.

“Tuungane, tujenge uchumi kwanza, tupigane na ufisadi, tuinue maisha ya mwananchi kiuchumi ili tuwe na pesa za kudai mishahara,” alisema.

Kiongozi wa ODM, Raila Odinga ambaye alihudhuria hafla hiyo, pia aliwasihi wauguzi kurejea kazini.