Habari Mseto

Msitu wa Mau kuzungushiwa ua kuanzia Aprili – Natembeya

January 6th, 2020 2 min read

Na SAMUEL BAYA

MPANGO wa kuweka ua kuuzunguka msitu wa Mau eneo la Narok utaanza Aprili, mratibu wa shughuli za serikali Bonde la Ufa, Bw George Natembeya alisema Jumapili.

Akiongea kwa simu, Bw Natembeya alisema kuwa utoaji zabuni kwa mpango huo utafanyika Machi baada ya zabuni hizo kutangazwa katika siku chache zijazo. Baadaye uwekaji wa ua huo utaanza Aprili hadi Julai.

“Tulichelewa kuanza mpango huu kwa sababu hatukuwa tumepata ripoti ya tathmini za kimazingira za msitu huo (EIA).

Lakini sasa ripoti imetolewa na utoaji zabuni utaanza karibuni. Tunalenga kuweka ua katika msitu huo wenye ukubwa wa kilomita 120,” akasema Bw Natembeya. Kulingana na afisa huyo, serikali itaweka ua katika umbali wa kilomita 50 kisha badaye mashirika mengine nayo yawekeze kwa kuweka ua katika sehemu ambazo zimebakia.

Hata hivyo mkuu huyo wa eneo alikosa kutaja kiwango cha fedha ambazo serikali itatumia kuweka ua huo, ila akastitiza kwamba ni muhimu msitu huo kulindwa kutoka kwa watu ambao wana uharibu.

“Wakati tukitoa zabuni, wakenya watajua ni fedha ngapi ambazo zitatumika katika kuweka ua, ila kwa sasa jambo muhimu ni kuwa lazima tuhakikishe kwamba msitu huo umelindwa kabisa,” akasema Bw Natembeya.

Mwaka jana, serikali ilianzisha awamu ya pili ya kuwafurusha wakazi ambao ambao walikuwa wamevamia msitu huo katika zoezi ambalo liliwezesha familia 60,000 kuondolewa katika msitu huo.

Kulingana na Bw Natembeya eneo ambalo lilikuwa limevamiwa wakazi katika msitu huo lilikuwa limeathiri jumla ya wakazi 10 millioni na kwamba lilikuwa eneo muhimu sana la serikali.

Kulingana na ripoti ambayo ilitayarishwa na shirika la kuhifadhi chemichemi za maji nchini(Kenya Water Towers Agency (KWTA) mwezi wa Septemba, serikali itawkea ua kuanzia eneo la Sierra Leone hadi eneo la Olkurto. Julai mwaka jana, waziri wa mazingira Bw Keriako Tobiko alitangaza mpango wa kuwafurusha watu katika msitu huo , jambo ambalo lilizua malumbano makali ya kisiasa.

Kwa sasa serikali inaendeleza upanzi wa miti 10 milioni ili kuulinda msitu huo usiharibiwe tena. Kufikia sasa zaidi ya hektari 14,000 za ardhi ndani ya msitu huo zilikuwa zimeharibiwa.

“Uvamizi wa msitu wa Mau ndio tishio kubwa ambalo linakumba msitu huo kwa sasa. Ni tatizo ambalo limekuwa likiendelea tangu miaka ya sabini wakati serikali ilipotangaza mipango ya makazi katika eneo hilo,” ikasema sehemu ya ripoti hiyo ya KWTA ambayo ‘Taifa Leo’ iliona.