Msomi akiri kukiuka maadili kwenye mahojiano ya Jaji Mkuu

Msomi akiri kukiuka maadili kwenye mahojiano ya Jaji Mkuu

Na RICHARD MUNGUTI

MSOMI wa masuala ya sheria anayeomba ateuliwe kuwa Jaji Mkuu, jana alifichua kwamba alitumia utafiti uliofanywa na msomi mwingine wa Chuo Kikuu cha Nairobi kupokea pesa kutoka kwa Wakfu wa Ford, akidai ndiye alikuwa ameufanya.

Profesa Kameri-Mbote, aliambia Tume ya Uajiri Idara ya Mahakama (JSC) aliungama kuwa aliwasilisha utafiti huo kwa wakfu huo wa Ford bila kumtaja mtafiti halisi katika ripoti hiyo, inavyohitajika katika maadili ya usomi na uchapishaji.

Msomi huyo aliambia JSC kuwa aliichambua ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) na kuishauri bunge kuhusu mchakato huo wa kufanyia katiba marekebisho.

Profesa Kameri-Mbote, aliambi Tume ya Uajiri Idara ya Mahakama (JSC) kuwa alipigiwa simu na kuombwa aisome kisha ataoe ushauri wake kwa bunge.

“Sitaki kuzungumzia suala hili la BBI kwa undani kwa vile kuna kesi inayoihusu ambayo haijaamuliwa na korti,” aliambia JSC.

Prof Mbote, ambaye alihojiwa na makamishna wa JSC chini ya uongozi wa kaimu mwenyekiti, Prof Olive Mugenda, alisema akiteuliwa kuwa Jaji Mkuu ataifanikisha Idara ya Mahakama hadi upeo wa juu mno kutokana na ujuzi mwingi alio nao wa usimamizi.

Kuhusu ukaidi wa maagizo ya mahakama na kutoapishwa kwa majaji 41, Prof Mbote alisema atatumia ukakamavu wake kusuluhisha shida zinazozonga Idara ya Mahakama na asasi zingine kwa njia ya mashauriano.

Alisema dhana kuhusu ufisadi mahakamani ndiyo mbaya kuliko uozo wenyewe, na atafanya kila awezalo kulisambaratisha endapo atateuliwa kuwa Jaji Mkuu.

Leo Jaji Martha Koome wa Mahakama ya Rufaa atahojiwa.

You can share this post!

Wizara yamtishia mwalimu aliyefichua masaibu yake

Ramadhan kupiga breki siasa moto za kumrithi Joho