Habari Mseto

Msongamano Krismasi: KeNHA yatangaza barabara mbadala

December 23rd, 2019 2 min read

Na WANDISHI WETU

MAMLAKA ya Barabara za Kitaifa Kenya (KeNHA) imetangaza barabara mbadala ambazo zitatumika wakati kutakapokuwa na msongamano katika barabara ya Nakuru-Narobi yenye shughuli nyingi.

Mkurugenzi wa KeNHA, Bw Peter Mundinia alisema hatua hiyo imechukuliwa kwa vile msongamano mkubwa hushuhudiwa katika barabara hiyo wakati wa sikukuu.

Kwenye taarifa, alisema watumiaji wa barabara ya James Gichuru hadi Rironi ambayo iko katika Southern Bypass wanaweza kutumia barabara ya Gikambura-Mutarakwa ama ile ya Gigiri-Ndenderu-Kamandura.

Katika eneo la kupimiwa uzani la Gilgil, madereva wanaweza kutumia barabara ya Flyover-Njabini-Engineer-Olkalou-Lanet ama Naivasha-Engineer-Olkalou had Lanet.

Mapema mwezi huu, abiria walilazimika kulala njiani baada ya msongamano mkubwa kutokea katika eneo la Gilgil.

Hayo yamejiri huku idadi ya wasafiri ikizidi kuongezeka na kufanya wenye magari ya uchukuzi wa umma kuongeza nauli.

Wamiliki wa magari ya binafsi mjini Nakuru wanatumia hali hiyo kujipatia mapato kwa kusafirisha wakazi kutoka mjini hadi maeneo tofauti nchini.

Jana asubuhi, vituo vingi vya mabasi vilishuhudiwa msongamano mkubwa wa abiria wanaosafi ili kujiunga na wapendwa wao walioko sehemu za mashinani.

Magari ya binafsi haswa ya aina ya Probox yamejitosa barabarani ingawa yanafanya kazi hiyo kwa siri kwani hairuhusiwi kisheria.

Katika vituo vya magari vya Kolen na Highway Towers kwenye barabara kuu ya Nakuru kuelekea Eldoret, magari mengi ya binafsi yameonekana yakiegeshwa sehemu hizo ambazo abiria wengi wa kuelekea maeneo ya Magharibi hulipia nauli zao.

Taifa Leo iligundua kwamba magari hayo yanaegeshwa kando mwa barabara kama kilomita kadha kutoka eneo la kuegesha magari ya usafiri na kisha abiria kuelekezwa hadi sehemu hiyo kwa njia mbayo si rahisi kutambulika na polisi.

Katika eneo la Pwani, abiria wengi walionekana kuchanganyikiwa katika vituo tofauti vya matatu baada ya wenye matatu kupandisha nauli.

Mwendo wa alasiri, abiria wengi walionekana katika steji kama vile Mtwapa, Shanzu na Bombolulu wakisubiri kupunguzwa kwa nauli.

Wakati huo huo, wamiliki wa kampuni za magari ya usafiri wa umma wameonywa dhidi ya kuweka magari mabovu barabarani na uendeshaji wa kiholela msimu huu wa likizo ili kuzuia ajali.

Mshirikishi wa eneo la Pwani, Bw John Elungata alisema wahudumu hutumia magari yasiyostahili kuwa barabarani ili kukidhi wateja wengi ambao wanasafiri kwenda maeneo mbali mbali ya nchi, kujumuika na familia zao kwa sherehe za Krisimasi.

“Tunawaonya madereva watakaobeba abiria kupita kiasi na kuendesha kwa mwendo wa kasi. Wahudumu watakaopatikana wameruhusu magari mabovu kubeba abiria pia watapokonywa vibali vya kuhudumu,” akasema.

Aidha alisema kampuni zaidi za mabasi ziko katika hatari ya kupoteza vibali vyao vya uhudumu, kwani maafisa wa usalama wameimarisha msako kwa wanaovunja sheria za trafiki msimu huu.

Alionya pia abiria dhidi ya kuabiri magari yaliyojaa akisema wkipatikana watachukuliwa hatua za kisheria.

“Tunawaomba, japo muna haraka ya kufika kwa familia zenu mapema tafadhali zingatieni usalama wenu. Maafisa wa polisi hawatasaza yeyote atakae kuwa amezidi katika gari la abiria, watu hawa ndio wanaosaidia madereva kuvunja sheria,” akasema.

Ripoti Za Samuel Baya, Phyllis Musasia, Mishi Gongo Na Charles Ongadi