Habari Mseto

Msongamano Likoni feri 3 zikiondolewa

November 30th, 2019 2 min read

Na MOHAMED AHMED

MAELFU ya watu wanaotumia kivuko cha Likoni watakuwa na wakati mgumu kusafiri hasa msimu huu wa likizo ya Krismasi kufuatia kuondolewa kwa feri kubwa ya MV Jambo.

Wageni wengi wanatumia kivuko hicho kwenda maeneo ya Pwani Kusini kwa ajili ya kujivinjari wakati wa likizo ya Desemba.

Jana, msongamano wa magari na watu tayari ulikuwa umeanza kushuhudiwa katika kivuko hicho cha jijini Mombasa kufuatia kuondolewa kwa feri hiyo ya MV Jambo ambayo ndio kubwa humu nchini.

Hali hiyo inajiri huku ikiwa tayari wageni kutoka pande tofauti za nchi na wale wa nchi za nje wameanza kumiminika katika kanda ya Pwani kwa ajili ya likizo ya Desemba.

Shirika la Huduma za Feri (KFS) limetangaza kuwa feri hiyo itaondolewa kwa muda wa wiki mbili, hivyo basi itatarajiwa kurudi kuhudumu katikati ya mwezi wa Desemba.

Ijumaa asubuhi tayari hali ilikuwa tete kivukoni hapo baada ya feri nyingine mbili ikiwemo MV Kwale na MV Nyayo kuondolewa.

Mlolongo wa magari ulishuhudiwa upande wa Likoni huku madereva wakilazimika kukaa zaidi ya saa moja na nusu kabla kuvuka.

“Nimekaa sana. Sidhani kama likizo nyingine nitakuja upande huu wa Kwale. Nimekuja hapa kuanzia saa tatu unusu na nimekaa hadi saa tano ndio navuka,” akasema afisa mmoja wa kuajiri walimu nchini ambaye alikuwa anavuka na feri ya Kilindini.

Feri zilizokuwa zinahudumu wakati huo ni ile ya MV Kilindini, MV Harambee na MV Likoni.

Feri hizo tatu zinajikokota kwa sababu ya ubovu wake hali ambayo imezidisha shida kivukoni hapo. Zile za MV Harambee na MV Kilindini zimetumika kwa muda miaka 30 sasa, hali ambayo imepelekea KFS kutaka ziondolowe.

Watumizi wa kivuko cha Likoni hata hivyo wamelalamika kuondolewa kwa feri hiyo wakati huu.

“Mbona muondoe feri ambayo inasaidia kupambana na msongamano wakati huu wa msimu wa likizo. Kutakuwa na shida kubwa sana. Tafakarini hilo,” akasema Musa Abdallah katika mtandao wa kijamii.

Kwa kawaida feri nne hadi tano ndio huhudumu kivukoni hapo na ndizo zenye uwezo wa kupambana na msongamano wa magari na watu.

Kila siku watu zaidi ya 350,000 na magari zaidi ya 6,000 hutumia kivuko hicho cha Likoni.

Wakazi wengine walikuwa wanatumia kivuko cha Mtongwe ambacho sasa kimefungwa kwa sababu ya marekebisho.

Marekebisho hayo yanatarajiwa kukamilika katikati ya mwaka ujao, kulingana na KFS.