Habari Mseto

Msongamano vituo vya mabasi Mombasa wageni wakirudi nyumbani baada ya likizo

January 2nd, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

KATIKA vituo vya mabasi mjini Mombasa kumefurika wasafiri wengi wakiwa ni wageni wanaorudi nyumbani na maeneo mengine ya nchi na hata nje ya nchi baada ya likizo ya Krismasi na sherehe za Mwaka Mpya mjini humo.

Wageni hao waliokuwa wamezuru Mombasa na maeneo mengine ya Pwani kwa likizo, wameelezea kero ya kupata usafiri na nauli za juu wanazotozwa.

Hata hivyo, wengi wao wameelezea kufurahia ukarimu wa watu wa Mombasa na uzuri wa mji wenyewe wa kikale.

“Nimefurahia sana kuwa Mombasa, ni mji unaopendeza. Hasa sehemu zilizonifurahisha ni Mji wa Kale, na Fuo za Bahari Hindi

Pia nimefurahia vyakula mbalimbali vikiwemo biriani, pilau, na viazi karai,” Bi Lilian Mambo amesema.

Naye Bi Dorcas Ambecha amelaumu wahudumu wa magari kwa kupandisha nauli maradufu kwa kutumia fursa ya kuwepo kwa wasafiri wengi.

“Kutoka Mombasa kwenda Webuye tulikuwa tunalipa Sh1800 nauli ya kawaida lakini sasa hivi tumetozwa Sh2500,” ameeleza Bi Ambecha.

Mwingine ni Bw Boaz Joseph anayewashutumu wahudumu hao kwa kuruhusu ‘wakora’ kuhudumu katika vituo hivyo.

“Nimekata tiketi kwa Sh2500 ambapo ninaenda Keroka, Kaunti ya Kisii; hii ni licha ya kwamba kwa tiketi hiyo nauli imeandikwa ni Sh1700 na hivyo inaonyesha kuwa tozo la juu linamfaidi mtu mwingine mbali na wamiliki wa mabasi,” amesikitika Bw Boaz Joseph.

Wamiminika

Wageni hao walianza kumiminika katika Kaunti ya Mombasa kuanzia mwezi wa Novemba na Desemba 2019.

Kaunti ya Mombasa inasifika kwa kuwa kitovu cha utalii nchini. Kwa sababu hii, watalii wa ndani kwa ndani na wale wa kutoka mataifa ya kigeni humiminika katika kaunti hiyo kwa likizo za Agosti na Desemba.

Ujio wa wageni hao katika mji huo umewafaidisha wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali, wakiwemo wa vyakula, leso, magari ya usafiri na sehemu za burudani.