Msongamano wa wagonjwa wazidi hospitalini

Msongamano wa wagonjwa wazidi hospitalini

Na STEVE NJUGUNA

AKINA mama wanaojifungua wamelalamikia msongamano wa wagonjwa kwenye wodi zao katika hospitali ya Kaunti ya Nyahururu, Laikipia.

Walisema kuwa kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika hospitalini humo, kitanda kimoja kinatumiwa na watu watatu.

“Hali ni mbaya kabisa. Kwa sasa tunalazimika kutumia kitanda kimoja wagonjwa watatu,” akasema mama aliyejifungua hapo.

Mhudumu mmoja wa katika hospitali hiyo alisema kuwa tatizo kubwa ni ukosefu wa nafasi.

“Hospitali hii ilikusudiwa ihudumie watu kutoka Laikipia Magharibi, lakini zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanatoka katika kaunti jirani za Baringo, Nyandarua na Subukia na Nakuru. Kwa kuwa hii ni hospitali ya umma hatuwezi kuwafukuza,” akasema mhudumu huyo.

Gavana wa Laikipia, Nderitu Muriithi alisema ujenzi wa hospitali mpya umefikia hatua muhimu na tatizo la sasa la msongamano litapungua kwa asilimia kubwa.

“Nimekuwa nikifuatilia ujenzi wa hospitali mpya ya Nyahururu ambayo itakuwa na vitanda 120 vya wagonjwa. Mwanakandarasi amenihakikishia kwamba ujenzi huo utakamilika kwa wakati na tatizo la sasa halitashuhudiwa tena,” akasema Bw Muriithi.

Hata hivyo, baadhi ya madaktari wamekashifiwa kwa kuwataka wagonjwa watafute huduma katika kliniki za kibinafsi.

Wiki jana, polisi wa Laikipia Magharibi walimnasa muuguzi akiwa na dawa zilizokuwa zimeibwa kutoka kituo cha afya cha Sosian katika kaunti hiyo.

You can share this post!

Nani huyo kawanyonga?

Murathe sasa apotosha bunge kuhusu wizi wa mabilioni ya...