Habari Mseto

Msongamano wa wanafunzi waathiri elimu ya chekechea

January 14th, 2019 2 min read

BENSON AYIENDA na LAWRENCE ONGARO

MASOMO yametatizwa katika baadhi ya shule za msingi za umma katika Kaunti ya Kisii kufuatia msongamano katika shule za chekechea na kusababisha walimu wengi kuamua kufunzia chini ya miti.

Mnamo 2016, kaunti hiyo ilikuwa imetangaza madarasa mawili ya chekechea yatajengwa katika kila shule ya umma na kuajiri walimu 1,000 zaidi.

Wanakandarasi waliopewa jukumu hilo la ujenzi sasa wamelaumiwa kwa kuchelewesha kazi hiyo iliyokwama katika maeneo mbalimbali ya kaunti kwa hali isiyoeleweka.

Imedaiwa walifanya kazi duni na baadaye wakashirikiana na baadhi ya maafisa wa kaunti kufuja hela zilizotengewa uimarishaji wa shule za eneo hilo.

Walimu wakuu wa shule za umma wakiongozwa na mkuu wa shule ya Nyanguru, Bi Magret Onduso, walitaka serikali ya kaunti itekeleze ahadi yake ya kukamilisha ujenzi wa madarasa.

Bi Onduso alisema katika shule yake pekee, kuna wanafunzi 234 wa chekechea ambao wamejazwa kwa darasa moja ambalo halijakamilika huku pia kukiwa na uhaba wa walimu na vifaa vya kufunzia.

“Tunaomba serikali ya kaunti ishughulikie suala hili kwa dharura kabla hali iwe mbaya zaidi,” akasema.

Awali, Waziri wa Elimu katika Kaunti, Bw Amos Andama, alisema serikali ya kaunti ilikuwa na mipango ya kuajiri walimu wengine 500 wa chekechea.

“Kaunti ya Kisii ina idadi kubwa zaidi ya walimu wa chekechea nchini na tunapanga kuajiri wengine 500 katika mwaka hu wa kifedha,” akasema.

Aliongeza kuwa madarasa ya chekechea yatafanyiwa ukarabati ili yafikie kiwango cha ubora kinachohitajika.

“Inafaa tukubali kuwa kuajiri walimu wa kutosha waliohitimu na ujenzi wa madarasa yaliyo na vifaa ni hatua kubwa itakayotuwezesha kuboresha hali ya elimu katika kaunti yetu,” akasema.

Kwengineko, wanafunzi karibu 600 kutoka eneo la Kamenu, Makongeni, mjini Thika, walinufaika na fedha za basari kutoka kwa diwani wao.

Akizungumza wikendi wakati wa hafla hiyo, Bw Raphael Chege alisema wanafunzi wa sekondari, wa vyuoni na walemavu walinufaika na Sh1.9 milioni za basari.

Alisema atalazimika kuongeza Sh1 milioni kwa sababu wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza wameongezeka.

Alitoa mwito kwa wazazi kuwa mstari wa mbele kuwashauri wana wao wanapowapeleka shuleni.

“Wazazi wanaowapeleka watoto wao hasa kidato cha kwanza wana changa moto kubwa kwa sababu watoto hao wanastahili kupewa mwongozo jinsi ya kukabiliana na maisha wanapofika shuleni,” alisema Bw Chege.

Alisisitisha umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi na viongozi kwa lengo la kudumisha umoja.

Bw Moses Mwaura ambaye ni mzazi alipongeza juhudi za serikali ya kutoa fedha kiasi za kusaidia wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni.

Aliwahimiza wazazi kushirikiana na viongozi kila mara ili kufanikisha maswala mengi ya maendeleo.