‘Msoto’ watisha kuyumbisha Gor mwaka mpya ‘21

‘Msoto’ watisha kuyumbisha Gor mwaka mpya ‘21

Na CECIL ODONGO

MASAIBU ya kifedha yanayoandama timu ya Gor Mahia hayaonekani kukoma hata katika mwaka mpya unaoanza hii leo, klabu hiyo ikiendelea kudaiwa pesa na wachezaji wa sasa na zamani.

Aliyekuwa kiungo wa mabingwa hao mara 19 wa ligi ya Kenya, Jackson Owusu, ni wa hivi punde kudai pesa zake.

Raia huyo wa Ghana amefichua kuwa ataishtaki K’Ogalo katika Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa kukataa kumlipa jumla ya Sh2.6 milioni.

Kiasi hicho cha hela kinajumuisha mshahara wa miezi saba, marupurupu ya kushinda mechi na ada ya usajili ambayo haikulipwa wakati Owusu alijiunga na Gor katika dirisha dogo la uhamisho wa wachezaji mnamo Januari 2020.

Owusu sasa hana klabu na anaendelea kuishi kwao Ghana.

Aliambia Taifa Leo kwamba hakulipwa hata shilingi moja ya mshahara alipokuwa akisakatia K’Ogalo, kabla ya msimu kusitishwa mnamo Machi 16, 2020, kutokana na mkurupuko wa corona.

“Tangu nijiunge nao na kuwachezea hawakuwahi kunipa mshahara wowote. Je, huduma zangu kwa Gor Mahia zilifaa kuwa za bure? Nimekuwa nikiwasiliana na uongozi wa klabu ili nilipwe fedha zangu lakini wamekuwa wakinipuuza tu.

“Sasa sina lingine kwani nimewasiliana na wakili wangu ambaye atapeleka kesi yangu FIFA,” Owusu akaeleza.

Kwa wakati mmoja mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 alizuiliwa katika hoteli ya Jimlizer mtaani Buruburu, Nairobi, baada ya K’Ogalo kukosa kulipa deni la Sh600,000.

Hatua ya Owusu kushtaki Gor kwa FIFA inajiri siku chache baada ya shirikisho hilo kuamuru K’Ogalo imlipe aliyekuwa winga wao na raia wa Tanzania, Dickson Ambudo, deni la Sh1.3 milioni.

Kwenye uamuzi huo, FIFA iliipa K’Ogalo siku 45 ilipe fedha hizo, la sivyo izuiwe kusajili wachezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi.

Madhila zaidi kwa K’Ogalo ni mgomo unaoendelea wa wachezaji wao ambao wanadai mshahara wa miezi miwli.

Wanasoka hao wametisha kususia mechi ya marudiano ya CAF dhidi ya CR Belouizdad mnamo Januari 6, 2021, iwapo hawatalipwa fedha zao.

You can share this post!

DOMO KAYA: Ama kweli yote ni vanity!

Swara tena EPL