Dondoo

Msupa akerwa na jombi wake kujitoa mapema baada ya polo sonko kuanza kummezea mate

May 7th, 2024 1 min read

NA NICHOLAS CHERUIYOT

MOLO, NAKURU

KIPUSA wa hapa alimkemea mpenziwe kwa kukubali kushindwa mapema na polo mmoja tajiri aliyemmezea mate.

Mdaku aliarifu kuwa kipusa na polo walianza uhusiano wa kimahaba juzi lakini mambo yaligeuka sonko mmoja aliomptamani kipusa.

“Sonko alimwambia polo waziwazi awe tayari kumenyana naye vikali na kushikilia atampokonya kipusa kwa njia rahisi,” mdaku akaarifu.

Polo aliingiwa na tumbojoto na akasalimu amri akilia hawezi kushindana na mdosi kwani yeye hana chochote.

Alipomfahamisha demu haya, kipusa alimsuta kwa kuwa mwoga kama kunguru.

“Kamwe sitakubali kuwa mpenzi wa sonko huyo. Siwezi kuhadaiwa kwa pesa. Wewe pia cheza mbali nami kwani sina nafasi ya mtu asiyejiamini,” kipusa akamsuta kalameni.