Mswada kudhibiti mikopo ya kidijitali waandaliwa

Mswada kudhibiti mikopo ya kidijitali waandaliwa

JOHN MUTUA Na SAMMY WAWERU

BUNGE limeidhinisha kujadili mswada unaolenga kudhibiti riba inayotozwa wateja wanaoomba mikopo kupitia mashirika au kampuni zinazotoa huduma za fedha kwa njia ya simu.

Endapo mswada huo utapita, pia utalinda wanaolemewa kulipa mikopo, kutokana na visa vya wateja kuhangaishwa na kampuni zinazomiliki apu hizo kuendelea kuripotiwa.

Wabunge wameashiria kutathmini sheria hizo na ambazo zikiidhinishwa kampuni na mashirika yanayotoa mikopo kwa njia ya simu yatakuwa chini ya uangalizi wa Benki Kuu Nchini (CBK).

Tayari Mswada huo wa CBK 2020 umewasilishwa katika Kamati ya Fedha Bungeni na ile ya Mpango wa Kitaifa, ambapo Wakenya na wadauhusika wataalikwa kutoa maoni kabla kupelekwa bungeni kujadiliwa kupitishwa au kuangushwa.

“Marekebisho hayo ya sheria yanapania kuzuia mtu yeyote, taasisi, kampuni au shirika kukopesha Wakenya pesa. Lazima wawe wameidhinishwa na CBK,” mbunge maalum Gedion Keter na ambaye ametoa mapendekezo hayo ameeleza kwenye notisi.

Kuna mashirika mengi ambayo hayadhibitiwi na CBK yamewekeza katika biashara ya kukopesha fedha.

Yametajwa kuendelea kukandamiza na kuhujumu wateja, kupitia kiwango cha juu cha riba inayotozwa. Inakadiriwa, kwa mwaka riba inayotozwa hupanda hadi asilimia 520.

Ni hatua ambayo imechangia ongezeko la wateja wanaolemewa kulipa, idadi kubwa ikiishia kuorodheshwa katika CRB – Shirika linalofuatilia rekodi ya wateja wa mashirika ya kifedha nchini.

Apu ya M-Shwari na inayomilikiwa na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kwa ushirikiano na benki ya CBA, ndiyo inaongoza nchini katika ukopeshaji wa fedha kwa njia ya simu.

Hutoza riba ya asilimia 7.5, kwa mwaka takwimu zikionyesha riba hiyo ikijumuishwa inakwea hadi 395.

Tala na Branch pia wanaorodheshwa katika listi ya mashirika na kampuni zinazotoa huduma za mikopo kwa njia ya simu, asilimia ya riba wanayotoza kwa mwaka ikiwa 152.4 na 132 mtawalia.

Hatua ya kudhibiti mashirika ya kifedha nchini inajiri mwaka mmoja baada ya serikali kuondoa sheria iliyokuwa imepitishwa kuyadhibiti.

Sheria hiyo ilipitishwa Septemba 2016, mashirika ya kibinafsi na benki zikionekana kupuuza wateja na wafanyabiashara wa mapato ya chini na yale ya kadri kwa hofu wangeshindwa kulipa.

You can share this post!

Seneti yapinga mbinu ya serikali kusaka mgao wa Sh370...

Maeneo hatari kwa usalama Mathare yaorodheshwa