Habari za Kitaifa

Mswada wa Fedha 2024 waendelea kukosolewa vikali

June 2nd, 2024 2 min read

NA SAMWEL OWINO

WADAU mbalimbali wameibua masuala makuu tata katika Mswada wa Fedha wa 2024 ambayo huenda yakafanya maisha ya Wakenya kuwa magumu zaidi iwapo sheria inayopendekezwa itapitishwa.

Haya yanajiri huku ushirikishwaji wa wananchi katika Mswada huo ukiingia siku ya tano mnamo Jumatatu.

Mswada huo unapendekeza kuanzishwa kwa asilimia 2.5 ya ushuru wa magari, kupandisha VAT ya mkate kutoka sufuri hadi asilimia 16 na marekebisho ya kifungu cha 51(2) cha kulinda data.

Tayari upinzani umesema mswada huo, ambao unatoa hatua za kuongeza mapato kwa serikali ya Rais William Ruto tayari utaumiza Wakenya.

Malalamishi mbalimbali yaliyowasilishwa bungeni yinaonyesha kuwa wadau wengi wanapinga ushuru wa magari kwani wanadai kuwa wamiliki wa magari ya kibinafsi ndio watakaoumia zaidi.

Takriban wadau 40 ambao kufikia sasa wamewasilisha maoni yao kuhusu Mswada huo wamedai kuwa hatua hiyo ni sawa na kutozwa ushuru mara mbili na pia ni adhabu kwa watu wanaomiliki magari ya kibinafsi.

Wanadai kuwa hawapati faida yoyote wakiendesha magari yao ya kibinafsi hivyo hawafai kulipa ushuru huo.

“Hili ni pendekezo ambalo litawalemea walipa kodi wengi, ambao tayari wanatozwa ushuru mkubwa,” Kampuni ya PKF Taxation Limited ilisema.

Kampuni hiyo pia ilionyesha wasiwasi wake juu ya Kifungu cha 51(2) cha Mswada kinachotaka kurekebisha Sheria ya Ulinzi wa Data kuhusiana na taarifa za kibinafsi pale inapohitajika kutathmini, kutekeleza, au kukusanya ushuru au ushuru wowote ilivyoainishwa katika sheria iliyoandikwa.

“Kwa kumruhusu kamishna kufikia data ya kibinafsi bila kufuata kanuni za ulinzi wa data, taarifa za kibinafsi za mtu binafsi zinaweza kufichuliwa na kutumiwa vibaya. Pendekezo hili linatoa mamlaka makubwa kwa kamishna,” kampuni hiyo iliongeza.

Pia ilipinga kifungu cha 35 (b) cha Mswada ambacho kinalenga kupandisha VAT ya mkate kutoka sifuri uliokadiriwa hadi asilimia 16.

“Hii itawafinyilia wananchi wa kawaida kwani baadhi yao wanategemea mkate,” kampuni hiyo ilisema.

Taasisi ya Wahasibu nchini (ICPAK) pia ilipinga ushuru wa magari ilionya kuwa hatua hiyo itakuwa na athari mbaya katika uchumi wa nchi.

“Kutokana na sera ya taifa ya kodi, lengo la ushuru wa bidhaa limekuwa ni kushughulikia bidhaa ambazo zina sifa mbaya za nje. Kutoza ushuru wa bidhaa kwenye huduma za kifedha tayari ni mzigo kwa walipa kodi na ongezeko zaidi litafanya gharama ya maisha kupanda kupindukia,” ICPAK ilisema.

Kwa upande wake, Chama cha Watengenezaji Bidhaa nchini (KAM) kilionya kwamba ushuru wa magari utaongeza mzigo kwa walipa kodi ambao pia wanatarajiwa kulipwa ushuru mbalimbali.

Kando na hayo, KAM pia ilipinga VAT ya mkate.

“Wengi wataendelea kuumia zaidi. Ikumbukwe kuwa wengi wanategemea mkate na kuupandisha bei yake ni kuwafinyilia Wakenya zaidi,” KAM ilisema.