Makala

MSWADA WA JINSIA: Mjadala waanza

November 21st, 2018 3 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE Jumanne walianza kujadili Mswada wa Marekebisho ya Katiba ambao ukipitishwa utatoa nafasi kwa wanawake zaidi kuteuliwa bungeni ili kutimiza hitaji la katiba kwamba angalau thuluthi moja ya wabunge wawa wa jinsi tofauti.

Idadi kubwa ya wabunge waliochangia mjadala huo waliunga mkono mswada huo wakisema kupitishwa kwake kutawezesha wanawake zaidi kuteuliwa bungeni.

Mswada huo, ambao uliwasilishwa rasmi bungeni na kiongozi wa wengi Aden Duale, unapania kuifanyika marekebisho kipengee cha 97 cha Katiba ili kubuni viti maalum vitakavyojazwa na wanawake watakaopendekezwa na vyama vya kisiasa kwa msingi ya idadi ya wabunge wavyo bungeni.

Mswada huo pia unalenga kuhakikisha kuwa angalau thuluthi moja ya nafasi za kuteuliwa hazinashikilia na watu wa jinsi moja.

“Mswada huu unalenga hasa kuhakikisha kuwa tunatimiza hitaji la kipengee 81 cha katiba kwamba angalau thuluthi moja ya nafasi katika asasi za umma zinashikiliwa na watu kutoka jinsi tofauti. Kwa hivyo, mswada huu haupaswi kuchukuliwa kuwa mswada wa wanawake pekee,” akasema Bw Duale.

Inakadiriwa kuwa endapo mswada huo utapitishwa mlipa ushuru atabebeshwa mzigo wa takriban Sh300 milioni kila mwaka kama gharama ya kukidhi mahitaji ongezeko la idadi ya wabunge.

Bw Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini alitoa witi kwa wabunge wenzake, haswa wanaume, kuunga mkono mswada huo ili kuzuia uwezekano wa Mkenya yeyote kuwasilisha kesi mahakamani kutaka bunge livunjwe.

Onyo hili pia lilitolewa na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) William Cheptumo na Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa.

Kulingana na katiba mtu yoyote anaweza kuwasilisha ombi kwa mahakama ya juu kuomba bunge livunjwe.

“Leo ni siku ya kihistoria kwa bunge la 12. Nawaomba tuunge mkono mswada huu kwa saba sote tulibebwa na mama zetu kwa miezi tisa,” akasema Bw Duale.

Wakati huu bunge la kitaifa lina upungufu wa wabunge 42, kwa sababu kuna jumla ya wabunge 75 waliochaguliwa na kuteuliwa, ilhali idadi hitajika ni 117.

Bunge la seneti nalo lina wanawake 21 kati ya jumla ya maseneta 67. Kwa hivyo, kuna upungufu wa maseneta wawili wa kike ili kufikia hitaji la kikatiba wa angalau masenta 23.

Duale alisema wakati huu, wanawake wametengwa katika uwanja wa siasa na wanahitaji kupigwa jeki ili katika chaguzi zitakazofuatwa wataweza kugombea viti vya kushindaniwa.

Alitoa mfano wa wabunge Maison Leshomo (Mbunge Mwakilishi wa Samburu), Naisula Leisuuda (Samburu Magharibi), Esther Korer (Laikipia Kaskazini) na Martha Wangare (Gilgil) ambao baada ya kuteuliwa katika bunge la 11 waliweza kupata nguvu ya kushindani nafasi cha kuchaguliwa na wakashinda.

Jaribio la Mbunge wa Kangema Muturi Kigano la kupuuzilia mbali mswada huo kama uliokiuka Katiba lilizimwa na Spika Justin Muturi, aliyeamuru mjadala uendelee.

Kigano alidai kuwa mswada huo unaingilia mamlaka wa wananchi kulingana na kipengee cha 1 cha Katiba na hivyo inapasa kuidhinishwa kupitia kura ya maamuzi.

Kiongozi wa wachache John Mbadi pia aliunga mswada unawasaidia wanawake kupata nafasi ya kuweza kuathiri utekelezaji wa sera za nchi. “Imetuchukua muda wa miaka minane kujaribu kupitisha mswada huu. Wakati huu sisi kama wabunge tunapasa kufanya kila tuwezalo kupitisha mswad huu,” akasema Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini.

Lakini Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alisema japo anaunga mkono haja ya wanawake kupewa nafasi ya uwakilishi katika asasi za umma kama vile bunge, pendekezo la mswada huo kwa uteuzi huo ufanywe na wakuu wa vyama vya kisiasa.

“Hatupinga haja ya wanawake kupata nafasi za uwakilishi katika bunge lakini hatutaki wakuu kupata nafasi ya kuteua marafiki zao. Wanawake wa kule mashinani wanafaa kupewa nafasi hizo,” akasema Bw Barasa.

Mbunge huyo alidai kuwa kuna Katibu Mkuu wa chama cha Kisiasa ambaye alijiteua kuwa mbunge maalum kando na kuwateua mkewe, na mama mkwe wake kuwa madiwani maalum.

“Ikiwa hali hii itaendelea kama inavyodhihiri katika mswada huo basi sheria hiyo ya usawa wa jinsi utakosa maana,” Bw Barasa akasema,

Naye Mbunge Maalam David Sankok alisema kuwa mswada huo ukipitishwa vigogo wa vyama hawafai kutumia nafasi hizo za uteuzi kuwatunuku wapenzi wao al maarufu “slay queen”.

“Naunga mkono mswada huu lakini haufai kutumia kuwezesha “maslay queens” kuteuliwa bunge. Kanuni iwekwe kuhakikisha kuwa wale wanaoteuliwa na wenye uwezo wa uongozi,” akasema, kauli ambayo iliwakasirisha wabunge wa kike.

Wabunge hao wakiongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Murang’a Sabina Chege walilamika kuwa Bw Sankok aliwadunisha wanawake kwa kuwaita “slay queens”.

Ikiwa mswada huo utapitisha idadi ya wabunge katika bunge la kitaifa itapanda kutoka idadi ya sasa ya 349 hadi 391 huku idadi ya wanachama wa seneti itapanda kutoka 67 hadi 71.

Ni wanawake watatu pekee walichaguliwa katika seneti katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Tayari baadhi ya makundi ya mashirika ya umma yamewasilisha kesi mahakamani yakitaka bunge livunjwe kwa kushindwa kupitisha sheria ya uwakilishi sawa wa kijinsia.

Sheria hiyo ilipasa kupitishwa ndani ya miaka mitano baada ya kuzinduliwa kwa katika mnamo Agosti 2010.

Jaribio la Bw Duale na aliyekuwa Mbunge wa Ainabkoi Samuel Chepkonga kutaka sheria hiyo ipitishwe ziligonga mwamba kwa kukosa uungwaji mkono kutoka idadi tosha ya wabunge, yaani angalau wabunge 233, kati ya wabunge 349.