Mswada wa Kura ya Maamuzi kupewa kipaumbele bungeni

Mswada wa Kura ya Maamuzi kupewa kipaumbele bungeni

Na CHARLES WASONGA

MSWADA wa Kura ya Maamuzi ni miongoni mwa miswada itakayopewa kipaumbele na Bunge la Kitaifa litakaporejelea vikao vyake kuanzia Jumanne wiki ijayo.

Mswada huo ambao umedhaminiwa na Kamati ya Bunge inayosimamia Utekelezaji wa Katiba (CIOC) unatoa mwongozo utakaofanikisha kufanyika kwa kura ya maamuzi kuhusu marekebisho ya Katiba kupitia BBI.

Tayari Mswada wa BBI uko katika mabunge 47 ya kaunti ambapo unahitaji kupitishwa na angalau mabunge 24 kabla ya kuwasilishwa katika bunge la kitaifa na seneti. Baada ya kushughulikiwa katika mabunge hayo mawili hatima yake itaamuliwa na raia katika kura ya maamuzi ambayo imeratibiwa kufanyika Juni mwaka huu.

Kwenye taarifa, karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai alisema vikao hivyo pia vitatumiwa kujadili masuala ya bajeti ya kitaifa.

Wabunge wanatarajiwa kuchambua na kupitisha Taarifa kuhusu Sera ya Bajeti (Budget Policy Statement-BPS) ya mwaka wa kifedha wa 2021/2021 na miswada kuhusu ugavi wa mapato.

“Kulingana na Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma 2012, taarifa ya BPS inapasa kuwasilisha na Hazina ya Kitaifa bungeni kufikia Februari 15, kila mwaka. Baada ya hapo taarifa hiyo itachambuliwa na Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti na Kamati zingine 15 kuhusu Idara za Serikali Kuu kabla kuwasilishwa kwa kikao cha bunge lote,” akasema Bw Sialai.

Kuidhinishwa kwa BPS kutatoa nafasi kwa kuwasilishwa na kupitishwa kwa Mswada wa Ugavi wa Mapato (DORB) na Mswada kuhusu Ugavi wa Mapato Baina ya Kaunti (CARA) katika mabunge yote mawili.

“Miswada hii ni miongoni mwa ile ambayo itapewa kipaumbele katika mabunge haya mawili katika awamu hii ya tano ya vikao vya bunge. Miswada mingine tisa ambayo imedhaminiwa na chama cha walio wengi pia itajadiliwa katika awamu hii ya vikao vya bunge,” Bw Sialai akaongeza.

Bunge pia watapata fursa ya kushughulikia miswada 15 iliyodhaminiwa na kamati mbalimbali pamoja na miswada 50 iliyoadhaminiwa na wabunge binafsi.

Wabunge pia wanatarajiwa kujadili ripoti ya kamati mbali mbali ambazo zinachunguza masuala yenye umuhimu wa kitaifa kama vile sakata ya Sh7.8 bilioni katika Mamlaka ya Dawa Nchini (KEMSA).

Bunge la Kitaifa pia litashughulikia na kupitia kalenda yake ya awamu ya tano ya vikao vyake, ambayo itazingatia hali iliyosababishwa na janga la Covid-19 na masharti ya kuzuia msambao wa homa hiyo hatari.

You can share this post!

Dkt Mutua awataka wanasiasa kuheshimu familia za waliofiwa

Raila asema Ruto aliarifiwa kuhusu handisheki na Rais