Habari MsetoSiasa

Mswada wa Punguza Mizigo wapata pigo mahakamani

July 31st, 2019 1 min read

Na SAM KIPLAGAT

MAHAKAMA Kuu imesimamisha mabunge yote 47 ya kaunti kujadili wala kupitisha mswada wa marekebisho ya katiba uliopendekezwa na Chama cha Thirdway Alliance, maarufu kama Punguza Mizigo.

Jaji James Makau alisimamisha pia chama hicho kisiwasilishe mswada huo kwa Spika wa Bunge la Taifa, hadi atakapoamua vinginevyo.

Jaji alisema maagizo aliyotoa yatadumu kwa siku 14 mpaka wahusika waliotajwa kwenye kesi hiyo wawasilishe majibu yao.

Bw Elias Mutuma aliyewakilisha Thirdway Alliance kortini alipinga hatua hiyo na kusema wamepewa chini ya siku moja pekee kuwasilisha majibu yao.

Wakili huyo aliambia mahakama kwamba wangepewa angalau siku tatu.

Alipotoa uamuzi wake, Jaji Makau alimwagiza Bw Mutuma kupeleka majibu yake kabla siku tano zikamilike na kesi itasikilizwa Agosti 13.

Ombi liliwasilishwa mahakamani na Bw David Kamau Ngari na shirika la International Economic Law Centre.

Waliotajwa kuwa wahusika ni Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), maspika wa Seneti na Bunge la Taifa, Thirdway Alliance na maspika 47 wa mabunge ya kaunti.

Bw Ngari alipinga mswada huo kwa msingi kuwa IEBC ilikiuka sheria kwa kudai kupokea, kuthibitisha na kuidhinisha mswada huo kisha kuupeleka kwa mabunge ya kaunti kujadiliwa na madiwani.

Aliendelea kudai kwamba mswada huo una sehemu zinazokiuka misingi mikuu ya katiba, hasa kuhusu mapendekezo ya kupunguza maeneobunge kutoka 290 hadi 47.

Anapinga pia pendekezo la kufanya Seneti kuwa kuu kuliko Bunge la Taifa.

Zaidi ya hayo, amedai mswada huo umepatikana kupitia ukusanyaji wa sahihi za wapigakura kwa njia haramu.