Habari MsetoSiasa

Mswada wa refarenda watua rasmi bungeni

June 5th, 2020 1 min read

NA DAVID MWERE

MSWADA wa  Refarenda 2020, hatimaye ulifikishwa rasmi katika Bunge la Kitaifa kwa mjadala Alhamisi alasiri.

Hii ilikuwa saa chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuondolea wananchi shaka kuwa Kenya itapiga kura ya maamuzi kuhusu katiba mwishoni mwa mwaka huu.

 

Mwasa huo, ambao unapendekeza kuziba nyufa katika katiba ya sasa kuhusu kuandaliwa kwa refarenda, ni juhudi za Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji wa Katiba na uliwasilishwa bungeni na mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni mbunge wa Ndaragua Bw Jeremiah Kioni.

Kuwasilishwa kwake kulitoa fursa kwa Spika Justin Muturi kuagiza mswada huo urudishwa kwa kamati hiyo ili umma ushirikishwe, mchakato ambao utapelekea kuwasilishwa kwa ripoti bungeni kwa mjadala.

Ingawa mswada huo unapendekeza kuandaliwa kwa refarenda siku sawa na ile ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, unaweza kubatilishwa katika hatua ya tatu ya kusomwa.

Kulingana na katiba ya sasa, uchaguzi mkuu unafaa kuandaliwa Jumanne ya pili ya mwezi Agosti ya kila mwaka wa uchaguzi, kumaanisha kuwa uchaguzi ujao utakuwa Agosti 9, 2022.

Bw Kioni amesema pendekezo la refarenda na uchaguzi mkuu kuandaliwa siku moja linalenga kupunguza gharama ya mchakato mzima.

“Tukisema tunaandaa refarenda sasa, itatugharimu fedha nyingi ambazo Hazina Kuu haina,” Bw Kioni alisema.