Habari Mseto

Mswada wa tohara ya wavulana kufadhiliwa na serikali jikoni

December 14th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HUENDA visa vya wavulana kufariki kwa kupashwa tohara na watu wasiohitimu vitapungua au kumalizika kabisa, ikiwa bunge la kitaifa litapitisha mswada ambao umeidhinishwa na Spika Justin Muturi.

Mswada huo ambao umedhaminiwa na Mbunge wa Kandara Esther Wahome (pichani) pia unapendekeza kwamba wavulana hao watahiriwe katika mazingira safi katika hospitali za umma, gharama ambayo italipiwa na serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

“Katika siku za hivi majuzi kumekuwa na visa vingi vya vijana kupoteza maisha yao baada ya kutahiriwa visivyo na watu wasiomudu shughuli hiyo. Hii ni ishara kwamba hakujakuwa na ushauri na mafunzo mwafaka kwa vijana ambao hupitishwa katika utamaduni huu, hali ambayo huwaacha mikononi mwa matapeli ambao huwadhuru,” akasema.

“Watu kama hawa wanaweza kuwaingiza wavulana hawa katika mienendo mibaya kama vile matumizi ya mihadarati, pombe na vitendo vingine vya uhali wakiwa umri mdogo. Ni uovu ambao mswada huu unalenga kuondoa,” Mbunge huyo wa chama cha Jubilee akaeleza kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Mnamo Novemba 2, 2018 mvulana ambaye alikuwa ametahiriwa alipatikana amefariki baada ya kudaiwa kupigwa na wanaume ambao walikuwa wakimfunza kuhusu masuala ya utu uzima kutokana na ugomvi kuhusu kuku

Juliano Kanyonyo, 15, alipatikana asubuhi amefariki asubuhi chumbani mwake na mamake ambaye alikuwa amekuwenda kumwamsha akanywe chai.

Matokeo ya upasuaji wa maiti yake yalionyesha kuwa damu iliganda kwenye ubongo wake.

Mamake Beth Nyambura alisema wanaume wanne walimtembelea mvulana huyo kwa lengo kumshauri kumpa ushauri nasaha walimpiga wakitaka awapa kuku wa jogoo ambaye hakuwapa wakati huo.

Visa kama hivyo vimekuwa vikiripotiwa katika kaunti za Kiambu na Meru na Kirinyaga katika siku za ambapo wavulana wamekuwa akijeruhiwa au kuuawa na “ngariba” feki.

“Kwa hivyo, nimeandaa mswada huu kwa lengo la kuwaokoa wavulana kama Kanyonyo ambaye anatoka eneo bunge langu. Na hii ndio maana Spika Muturi ameuidhinisha,” akasema Bi Wahome.

Mbunge huyo alisema mswada wake utajadiliwa mwaka ujao, wabunge watakaporejea kutoka likizo ya Krismasi na Mwaka Mpya.

“Nina imani kwamba wabunge wenzangu, hasa wa kiume wataunga mkono mswada huu unaolenga kumnusuru mtoto mvulana,” akasema.