Habari Mseto

Mswada waibua kiwewe kwa walanguzi wa dawa

November 23rd, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

MSWADA wa sheria za kupambana na ulanguzi wa dawa za kulevya uliopendekezwa umezua tumbo joto miongoni mwa walanguzi kwa sababu ya adhabu kali zilizomo.

Viongozi wengi kutoka Pwani wanaupigia debe mswada huo wakitaka upitishwe kwa manufaa ya wananchi.

Mswada huo tayari upo katika mipango ya mwisho na wabunge wanaouskuma wanataka kuhakikisha unapita kabla mwaka ujao.

Taifa Leo imebainisha kuna wasiwasi miongoni mwa wale ambao wanaendeleza bishara hizo haramu.

Mahojiano na wadokezi walio na ufahamu katika ulanguzi wa mihadarati yalifichua kuwa baadhi yao wameanza kutafuta njia za kujaribu kukwamisha mswada huo usipitishwe bungeni.

Kulingana na mswada huo walanguzi wa dawa za kulevya watapata faini ya kati ya Sh50 milioni hadi Sh100 milioni iwapo utapitishwa.

Walanguzi ambao wapo nje ya Kenya wakipatikana wanashirikiana na wale walio nchini watapewa faini hiyo ya Sh100 milioni ama kifungo cha maisha, kulingana na kipengee ambacho kinasema kuwa mtu huyo atachukuliwa ni kama amefanya makosa hayo humu nchini.

“Iwapo mtu atapatikana na gramu 101 ya dawa za kulevya ama zaidi, basi atapata faini isiyopungua Sh50 milioni ama mara tatu ya thamani ya dawa hiyo na kifungo cha maisha,” kinasema kipengee kingine cha mswada huo.

Chini ya sheria ya sasa, walanguzi hupewa faini isiyozidi Sh1 milioni ama mara tatu ya thamani ya dawa ambazo wamepatikana nazo wakati wanapofikishwa mahakamani.

Vile vile, maafisa wa polisi ambao watapatikana kushiriki kwenye biashara hiyo kwa kusaidiana na walanguzi watapewa faini ya hadi Sh20 milioni ama kutumikia kifungo kisichopongua miaka 20 iwapo watapatikana kwenye hatia hiyo na mahakama.

Viongozi wa kisiasa na kidini katika kanda ya Pwani wameunga mkono mswada huo na kusema kuwa utasaidia kanda hiyo ambayo imeathirika pakubwa na janga hilo la dawa za kulevya.

Aidha, viongozi hao wamesema kuwa yoyote yule atakayepinga mswada huo basi atakuwa msaliti wa kizazi cha Pwani.

Mbunge wa Nyali Mohammed Ali ambaye amekuwa msatari wa mbele katika kupambana na walanguzi alisema kuwa mswada huo unalenga pakubwa kupambana na walanguzi wakubwa.

“Huu ndio wakati wa kupambana walanguzi hao wakubwa. Tutaanza mwaka mpya tukiwa na mswada huo mpya ambao utaruhusu faini hizo za juu na kuwezesha maafisa kupata ushahidi wa ndani zaidi dhidi ya wale wanaoshukiwa kuendeleza biashara hii haramu,” akasema.

Bw Ali aliongeza kuwa walanguzi wa dawa za kulevya kwa muda sasa wamekuwa wakijitajirisha kwa sababu ya kuwa na sharia hafifu dhidi yao.

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir kwa upande wake alisema kuwa yeyote ambaye atapinga mswada huo basi anapaswa kuchunguzwa ili itambulike ni kwa nini anafanya hilo.

“Mtu ambaye atakataa mlanguzi wa dawa za kulevya amepewe faini ya juu basi kutakuwa na maswali dhidi yake. Wale ambao watafanya hivyo basi wamulikwe,” akasema.

Katibu mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini Kenya (CIPK) Sheikh Mohammed Khalifa alisema kuwa mswada huo unaleta matumani katika kupambana na vita dhidi ya madawa ya kulevya.

Sheikh Khalifa alitoa mwito kwa mahakama, afisi ya mashtaka ya umma na afisi ya uchunguzi wa jinai kufanya kazi pamoja ili kuwezesha kulishinga janga hilo ambalo alisema limeangimiza vijana wengi hususan Pwani.

“Iwapo kutakuwa na mswada huo alafu kuwe na ushirikiano katika afisi hizo ambazo nimezitaja basi kutakuwa na mwelekeo humu nchini utakaowezesha kuwashinda maadui wa vizazi vyetu,” akasema.