Mswada walenga kupandisha hadhi lugha ishara

Mswada walenga kupandisha hadhi lugha ishara

Na CHARLES WASONGA

LUGHA ya ishara itapandishwa hadhi na kuwa lugha ya tatu rasmi nchini Kenya ikiwa mswada uliopitishwa wiki hii utatiwa saini kuwa sheria.

Mswada kuhusu Lugha ya Ishara ya Kenya unapendekeza kuwa lugha hiyo itumike katika afisi zote za serikali, shule na mahakama. Hii ni kando na lugha za Kiingereza na Kiswahili.

Mswada huo, ambao ulipitishwa Jumanne katika seneti pia unalenga kuhakikisha kuwa wanafunzi viziwi wanapewa nafasi sawa na wanafunzi wengine ili wawe watu wenye manufaa katika jamii.

“Waziri wa Elimu atahakikisha kuwa wanafunzi viziwi ambao wana matatizo ya kusikia wanafundishwa kwa njia ambapo wanaweza kuelewa na kutumia lugha inayotumiwa katika mafunzo shuleni,” mswada huo unasema.

Hii ina maana kuwa lugha ya ishara itafunzwa katika taasisi za elimu ya kimsingi, vyuo vya kadri na vyuo vikuu. Vile vile, lugha hii itafunzwa katika vyuo vya kiufundi sambamba na masomo mengine.

“Vile vile, lugha ya ishara itakuwa lugha ya lazima itakayofundishwa shuleni kando na Kiswahili na Kiingereza,” mswada huo unaeleza.

Mswada huo ulidhaminiwa na maseneta Gertrude Museruve (Seneta Maalum) na Margaret Kamar (Uasin Gishu).

Baada ya kupitishwa katika Seneti, mswada huo sasa utawasilishwa kwa bunge la kitaifa ili ujadiliwe na upigiwe kura.

Mswada wa Lugha ya Ishara ya Kenya unalenga kufanikisha utekelezaji wa kipengele cha 54 (d) cha Katiba kinachosema kuwa watu wanaoishi na ulemavu wana haki ya kutumia lugha ya ishara au mbinu zozote zile za mawasiliano.

“Lengo la mswada huu ni kuwezesha wanafunzi wenye matatizo ya kusikia kupata elimu bora,” inasema sehemu ya mswada huo.

Akitetea mswada huo, Seneta Museruve, ambaye anawakilisha watu wanaoishi na ulemavu, alisema baada yake kuwa sheria, taasisi za umma zitalazimika kuweka vifaa vya kuwasaidia watu walio na matatizo ya kusikia.

“Kwa hivyo, naomba wenzetu wa bunge la kitaifa kupitisha mswada huu bila kuufanyia mabadiliko ili wanafunzi wasio na uwezo wa kusikia wapate kusaidika,” akasema.

You can share this post!

Timbe aongoza Buriram kurukia uongozi wa Ligi Kuu Thailand

MALEZI KIDIJITALI: Mbinu za kudhibiti vifaabebe

T L