Habari Mseto

Mswada wanuia kuepusha Wakenya kuhangaikia vyeti muhimu

May 26th, 2024 2 min read

Na ERIC MATARA

WAKENYA hawatajisumbua tena kupata vyeti muhimu iwapo Mswada wa Usajili wa Wanaozaliwa na Wanaoaga Dunia 2024 utapitishwa bungeni.

Mbunge wa Gilgil Martha Wangari amewasilisha mswada huo ambao unalenga kuhakikisha cheti cha kuzaliwa na kile cha kifo kinatolewa katika maeneobunge yote 290.

Kwa sasa Kenya ina vituo 158 vya kutoa vyeti vya kuzaliwa na wanaofariki katika maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo, vituo hivyo vipo sehemu mbalimbali na hivyo husababisha Wakenya kusafiri umbali ili kuvipata.

Mfano ni Kaunti ya Nakuru ambapo ina watu zaidi ya milioni mbili lakini ina vituo vinne vinavyotoa vyeti vya kuzaliwa na vya kifo. Mswada wa Bi Wangari unalenga kumlazimisha Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki kuanzisha angalau afisi moja ya kutoa vyeti vya kifo na kile cha kuzaliwa kwenye kila eneobunge.

Mswada huo ukipita, Wakenya watapata huduma hizo katika afisi 132 zaidi za usajili wa vyeti vya mauti na kuzaliwa. Hata wakazi kutoka kaunti ambazo zimetelekezwa kwa miaka mingi nao hawatatatizika wakisaka huduma hizo.

Bi Wangari anasema mswada huo unalenga kupeleka huduma karibu na raia kwenye maeneobunge 290. Akiwa mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Usalama na Utawala, Bi Wangari alisema kuwa cheti cha kuzaliwa na kile cha kifo, ni stakabadhi muhimu ilhali Wakenya hutatizika sana kuzipata.

“Kuwa na maafisa katika maeneo ya mashinani wanaohusika na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na mauti, kutasababisha mchakato wote wa kutolewa kwao kuendelea bila tatizo lolote. Wakenya wamekuwa wakisafiri kwa kilomita kadhaa kupata vyeti hivyo,” akasema Bi Wangari.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, kuchelewa kutoa stakabadhi hizo kumesababisha wanafunzi kutatizika wanapojisajili kwa mitihani.

“Ni stakabadhi ambayo inahitajika sana shuleni na husababisha baadhi ya wanafunzi kuchelewa sana hata kujisajili kwa mitihani ya kitaifa,” akaongeza. Wanafunzi huhitajika kujisajili kwa mtandao wa Nemis kwa kutumia cheti chao cha kuzaliwa chenye nambari maalum.

Aidha mbunge huyo amesema kuwa afisi hizo mpya hazitakuwa mzigo mkubwa kwa walipa ushuru kwa sababu ziitakuwa na msajili, naibu msajili na karani.

Iwapo utapitishwa, serikali itatumia Sh219 milioni mwaka wa kwanza ambapo afisi hizo zitaanzishwa. Mwenyekiti wa kamati hiyo Dido Rasso ambaye ni mbunge wa Saku amesema kuwa wataupiga msasa mswada huo na kufanya marekebisho kabla ya kuuwasilisha bungeni.