Michezo

MSWAKI: Vikosi vya Uingereza kuwa na mteremko

October 22nd, 2019 3 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

VIKOSI vya Uingereza vitakuwa na mteremko mkubwa katika kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kitakachoingia raundi ya tatu ya hatua ya makundi hii leo Jumanne.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Manchester City watakuwa wenyeji wa Atalanta ya kutoka Italia ugani Etihad huku Tottenham Hotspur wakiwaalika Crvena almaarufu Red Star Belgrade ya Serbia katika Kundi B.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City kwa sasa wanaselelea kileleni mwa Kundi C kwa alama sita kutokana na michuano miwili dhidi ya Dinamo Zagreb na Shakhtar Donetsk. Atalanta waliopoteza michuano miwili ya ufunguzi dhidi ya Zagreb na Donetsk, wanakokota nanga mkiani mwa kundi.

Man-City wanapigiwa upatu wa kukizamisha chombo cha Atalanta kwa urahisi hasa ikizingatiwa ukubwa wa hamasa iliyowashuhudia wakiwapepeta Crystal Palace 2-0 katika kipute cha EPL wikendi iliyopita.

-Hadi waliposajili ushindi huo muhimu uliowasaidia kupunguza pengo la alama kati yao na viongozi Liverpool, Man-City walikuwa wamepoteza michuano miwili ligini dhidi ya Norwich City na Wolves.

Sare ya 1-1 ambayo Liverpool walilazimishiwa na Manchester United uwanjani Old Trafford mwishoni mwa wiki iliyopita ilipunguza pengo la pointi kati ya vijana wa Guardiola na wa kocha Jurgen Klopp hadi kufikia sita pekee. Liverpool ambao kesho watakuwa wageni wa Genk nchini Ubelgiji, kwa sasa wanajivunia alama 25 kileleni mwa jedwali la EPL.

Man-City walianza kampeni yao katika kipute cha UEFA msimu huu kwa kuwapokeza Donetsk kichapo cha 3-0 ugenini kabla ya kuwachabanga Zagreb uwanjani Etihad mwanzoni mwa mwezi huu.

Japo majeraha yanayouguzwa na baadhi ya mabeki wa Man-City yamewatatiza pakubwa kufikia sasa muhula huu, Guardiola amewataka vijana wake kujituma vilivyo na kutia kapuni alama muhimu zitakazoweka hai matumaini yao ya kumaliza kileleni mwa kundi na hivyo kukutana na mpinzani mnyonge katika hatua ya 16-bora.

Msimu jana, Man-City walibanduliwa na Tottenham Hotspur kwenye UEFA katika hatua ya robo-fainali. Hatua bora zaidi ambayo kikosi hiki kimewahi kufikia katika historia ya UEFA ni nusu-fainali mnamo 2015-16.

Kwa upande wao, huu ni msimu wa kwanza kwa Atalanta kunogesha kivumbi cha UEFA baada ya kuambulia nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mwishoni mwa muhula uliopita.

Ingawa mafanikio hayo ya Atalanta yatadumu kwa kipindi kirefu katika kumbukumbu za mashabiki wao, ukweli ni kwamba kikosi hicho kinapitia wakati mgumu katika soka ya UEFA.

Katika mechi yao ya kwanza, walipokezwa kichapo cha 4-0 kutoka kwa Zagreb kabla ya kupepetwa 2-1 na Donetsk mapema mwezi huu. Ugumu wa kibarua chao unazidishwa na ulazima wa kukutana na Man-City katika mechi mbili zijazo za UEFA.

Chini ya kocha Gian Piero Gasperini, Atalanta kwa sasa wanajivunia alama 17 kutokana na mechi nane, matokeo ambayo yanawasaza katika nafasi ya tatu nyuma ya Juventus na Inter Milan wanaojivunia alama 22 na 21 mtawalia.

Kikubwa zaidi kinachowaaminisha Atalanta ni kwamba wamepoteza mechi tatu pekee kati ya 16 za hadi kufikia sasa katika soka ya bara Ulaya ambayo imewashuhudia wakivuna ushindi mara saba. Aidha, wanajivunia rekodi ya kuwahi kuwaponda Everton 5-1 katika hatua ya makundi kwenye soka ya Europa League mnamo 2017-18.

Kukosekana kwa beki Aymeric Laporte kambini mwa Man-City kunamsaza Guardiola katika ulazima wa kuendelea kutegemea huduma za madifenda John Stones, Kyle Walker na Nicolas Otamendi ambao wanatarajiwa kushirikiana vilivyo na viungo Rodri na Fernandinho. Sergio Aguero anatatazamiwa kuongoza safu ya mbele ya Man-City watakaompumzisha kiungo matata David Silva.Katika mechi nyinginezo za leo, Donetsk watamenyana na Zagreb katika Kundi C huku Olimpiacos ya Ugiriki ikishuka dimbani kupimana ubabe na miamba wa soka ya Ujerumani, Bayern Munich katika Kundi B.

Atletico ya kocha Diego Simeone nchini Uhispania itakwaruzana na Bayer Levekusen ya Ujerumani katika Kundi D litakalowashuhudia pia Juventus wakiwaalika Lokomotiv Moscow kutoka Urusi.

Katika Kundi A, Paris Saint-Germain (PSG) watakuwa wageni wa Club Brugge nchini Ubelgiji huku Real Madrid wakiwaendea Galatasaray nchini Uturuki.