Michezo

Mt Kenya United yachomwa 7-2 na Nairobi Stima

February 24th, 2020 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Mt Kenya United ilichomwa magoli 7-2 na Nairobi Stima kwenye mechi ya Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL), nayo Bidco United ilitwaa pointi tatu muhimu ilipobeba bao 1-0 dhidi ya Modern Coast Rangers.

Nao wanasoka wa Kibera Black Stars (KBS) walifanya kazi ya ziada ambapo walitandika Shabana FC mabao 3-2.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, matumaini ya Ushuru FC kutwaa alama tatu muhimu yaligonga ukuta ilipozabwa mabao 2-1 na Fortune Sacco.

Nairobi Stima inayofunga tatu bora kwa alama 45, mbili mbele ya Vihiga United iliteremsha mechi safi mbele ya wapinzani wao na kusajili ufanisi huo kupitia Patrick Mugendi alipopiga hat trick, Levian Ochieng alitikisa nyavu mara moja huku Mokaya Douglas na Michael Onyango kila mmoja akiitingia bao moja.

Nayo mabao ya Mt Kenya yalijazwa kimiani na Tevin Opondo.

Naye David Orem aliifungia Bidco United bao lililoibeba kuzoa alama tatu muhimu na kuendelea kufunga tatu bora kwenye jedwali. Erick Odhiambo wa KBS alitupia mabao mawili naye Wilson Mwenda aliifungia bao moja.

Nayo mabao ya Shabana FC yalipatikana kupitia Fred Nyakundi na Victor Matete.

Kwenye mfululizo wa mechi hizo, Murang’a Seal ilitoka sare ya bao 1-1 na Coast Stima, Kenya Police ilirarua FC Talanta mabao 3-1, St Josephs Youth iliagana bao 1-1 dhidi ya Vihiga United nayo Administration Police ilizimwa bao 1-0 Vihiga Bullets.