Michezo

Mt Kenya, Vihiga washuka ngazi, Bandari namba 2

May 30th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

LIGI Kuu ya Kenya (KPL) inayodhaminiwa na kampuni ya kamari ya SportPesa ilimalizika jana katika viwanja mbalimbali, huku timu za Mount Kenya United na Vihiga United zilizomaliza katika nafasi mbili za mwisho zikishuka hadi daraja ya Supa Ligi.

Wakati timu hizo zikiteremshwa, Gor Mahia ambao waliibuka mabingwa wa ligi hiyo baada ya kutwaa ushindi zikisalia mechi tatu, hii ikiwa mara yao ya 18 kuibuka mabingwa, waliagana sare tasa ya mabao 2-2 na Mathare United.

Bandari walimaliza katika nafasi ya pili baada ya kuagana 2-2 na Nzoia Sugar jana katika mechi yao ya mwisho, wakifuatiwa na Sofapaka walioubuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Kakamega Homeboyz katika mechi iliyochezewa Kenyatta Stadium mjini Machakos.

Ulinzi Stars walijipa ushindi wa bwerere uwanjani Afraha jana baada ya Mount Kenya United kufika ugani humo wakiwa wamechelewa.

Hii ni mara ya tatu kwa vijana hao kugawa pointi za bwerere baada ya hapo awali kuzitunuku timu za Gor Mahia na Mathare United.

Mechi hiyo ilitakiwa kuanza saa nane lakini ikaahirishwa ili ianze saa tisa na dakika 45, lakini hata kufikia wakati huo walikuwa hawajafika uwanjani humo.

Hatimaye walifika huku wakiwa wamevalia nguo nyekundu ambazo pia zilikuwa zimevaliwa na wenyeji.

Mwamuzi wa mechi hiyo, Anthony Oweyo na wasaidizi wake Anne Njambo na Elizabeth Njoroge walisisitiza lazima wageni hao wabadilishe mavazi, lakini hawakufanya hivyo.

Tuzo ya mfungaji bora

Ulinzi walikuwa wameingojea mechi hiyo kwa hamu huku wakiitegemea kumwezesha mshambuliaji wao, Enosh Ochieng aliyefunga mabao 17 kufunga mabao ya kumwezesha kutwaa Kiatu cha Dhahabu.

Mshindi wa tuzo hiyo ni Allan Wanga wa Kakamega Homeboyz ambaye alifikisha mabao 18 kutokana na mechi 33. Nyota huyo wa zamani AFC Leopards alitawazwa mhsindi ugani Mbaraki SC licha ya kutofunga bao lolote kwenye mnechi ambayo walichapwa 2-0 na wenyeji, Bandari FC.

Posta Rangers waliomaliza katika nafasi ya 16 (tatu kutoka mkiani) baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Tusker, watashiriki katika mechi ya mchujo wa kuwania nafasi ya kubakia ligini.