Habari Mseto

Mtaa wa Kitisuru kupigwa mnada baada ya kampuni iliyoujenga kelemewa na deni

February 13th, 2018 1 min read

Afisa wa kampuni iliyojenga mtaa huo alidinda kufichua benki inayowadai pesa hizo. Alitaja hali ngumu ya uchumi kama sababu ya kushindwa kulipa mkopo. Picha/FOTOSEARCH

BERNARDINE MUTANU

MTAA wa kifahari wa Kitisuru unanadiwa na madalali kutoka Nairobi, baada ya kampuni inayojenga mtaa huo kushindwa kulipa mkopo.

Ujenzi wa mtaa huo uligharimu Sh1.19 bilioni. Katika notisi, madalali, Valley Auctioneers wamewaalika wanunuzi kufika kwa shughuli ya kunadi mtaa huo Februari 15.

Kutokana na hilo, huenda wawekezaji waliolipa pesa kabla ya majumba kujengwa wakapoteza pakubwa.

Mtaa huo umejengwa eneo la Kabete, Kaunti ya Kiambu katika shamba la ekari 5.23 na una majumba ya vyumba vitatu vya kulala kufikia 119 kulingana na notisi hiyo.

Wanaoazimia kununua majumba hayo wanahitajika kulipa robo ya gharama ya mauzo ya majumba hayo kwa hundi ya benki siku ya mnada na kulipa pesa zitakazobakia katika muda wa siku 60.