Habari Mseto

Mtaala mpya uko sambamba, haujakwama – KICD

October 8th, 2018 2 min read

 Na BENSON MATHEKA

MAGEUZI yanayofanyiwa mtaala mpya wa elimu hayajakwama, mkurugenzi wa taasisi ya kukuza mitaala nchini (KICD) Dkt Julius Jwan amesema.

Kwenye taarifa yake Jumapili, Dkt Jwan alipuuza madai kwamba utekelezaji wa mtaala huo umekumbwa na visiki na kusema hakuna mipango ya kuanza mfumo huo upya baada ya wizara ya elimu kufichua kwamba utekelezaji umefaulu. “Madai kwamba mageuzi yamekwama ni ya kupotosha na yamenuiwa kuzua hofu isiyofaa,” alisema Dkt Jwan.

Mkurugenzi huyo alisema mfumo wa utekelezaji unaoendelea ni unaokubalika kote ulimwenguni.

Alisema utathmini uliofanywa na kamati tekelezi iliyohusisha washika dau kutoka sekta tofauti ulifichua kwamba utekelezaji unaridhisha.

Ripoti hiyo, alisema, inaonyesha kuwa kiwango cha ubora wa mfumo huo ni asilimia 56 dhidi ya kiwango cha chini kinachokubaliwa kimataifa ambacho ni asilimia 50.

Kamati hiyo inasimamiwa na Waziri wa Elimu, Dkt Amina Mohamed na wanachama wake wanatoka wizara kadhaa za serikali, mashirika ya wataalamu, vyama vya walimu, vyama ya wafanyakazi, tume ya elimu ya juu, mashirika ya kidini, mashirika ya kijamii na sekta ya kibinafsi nchini.

Mashirika ya vijana, vyuo vikuu, wanahabari na mashirika wafadhili pia yamewakilishwa.

“Zilikuwa habari za kupotosha na kama ripoti nyingine ile, changamoto zimegunduliwa ambazo zinashughulikiwa ili kuhakikisha mtaala huo utazinduliwa rasmi mwaka ujao,” alisema Dkt Jwan.

Kwenye mkutano wa kamati tekelezi ya kitaifa, waziri Amina aliahidi kuwa serikali itatoa vifaa vya kufanikisha mtaala huo kwa shule zote.

Dkt Jwan alisema kwamba hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu mtaala huo. Aliwataka walimu wa madarasa ya juu kuwa watulivu wakisubiri fursa yao ya kufunzwa utekelezaji wa mtaala huo.

Kulingana na Dkt Jwan mtaala huo unatelekezwa kwa awamu na kwa hivyo walimu watapatiwa mafunzo huku utekelezaji ukiendelea hadi wale wa madarasa ya juu.

Kufikia sasa, walimu 160,000 wamepatiwa mafunzo na KICD yanayolenga walimu wa darasa la kwanza hadi la tatu.Alisema utathmini ni wa kuhakikisha mtaala ni wa kiwango cha juu.