Habari

MTAALA MPYA: Vurugu walimu wakimkaidi Sossion

April 24th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

VURUGU zilikumba uzinduzi wa mpango wa kitaifa wa kuwapa mafunzo walimu kuhusu mtaala mpya wa elimu wa 2-6-6-3, huku walimu wakimkaidi katibu mkuu wa chama chao (KNUT), Wilson Sossion.

Katika kaunti za Mombasa na Uasin Gishu, walimu walimkemea Bw Sossiojn na kuusifu mpango huo wa masomo wakisema, utakuwa muhimu sana kwa mustakabali wa wanafunzi

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Shule za Msingi (KEPSHA) Uasin Gishu, Bi Alice Kirui, aliwataka viongozi wa kitaifa wa KNUT wakome kuingiza siasa katika mpango huo.

Mnamo Jumatatu, Bw Sossion aliwaagiza walimu kote nchini wasihudhurie mafunzo hayo hadi masharti aliyotoa yazingatiwe na Wizara ya Elimu.

Katika kujaribu kuwazuia walimu wasihudhurie mafunzo hayo yaliyozinduliwa jana na Waziri wa Elimu, Profesa George Mahoga, baadhi ya maafisa wa KNUT walivamia vituo vya uzinduzi na kuzua fujo.

Katika Kaunti ya Kakamega, afisa mmoja wa KNUT alikamatwa kwa kuwaongoza wenzake kuvuruga shughuli ya utoaji mafunzo katika eneo hilo.

Katibu wa tawi la Kakamega ya Kati wa chama hicho, Tom Ingolo alikamatwa alipojaribu kuvuruga shughuli hizo katika Shule ya Msingi ya Shikoti.

“Polisi wamenikamata nilipoingia katika shule hiyo. Wanataka kunipeleka katika seli. Ninataka kuelezwa sababu yangu kukamatwa,” akasema Bw Ingolo.

Hali ya mkanganyiko pia ilishuhudiwa katika Shule ya Msingi ya Kakamega, baada ya maafisa wa chama hicho kuvamia vituo vya kutoa mafunzo na kuharibu baadhi ya vifaa. Katika Kaunti ya Makueni, mpango huo haukufaulu, baada ya maafisa wa KNUT kuwafurusha walimu waliokuwa katika vituo vya kutolea mafunzo.

Visa hivyo vilivyofanyika katika vituo vingi vilimfanya Kamishna wa Kaunti hiyo, Maalim Mohammed kutoa onyo kali kwa maafisa wa chama hicho.

“Hatutamvumilia yeyote anayevuruga mpango huu wa serikali,” akasema Bw Maalim. Walimu waliozungumza na ‘Taifa Leo’ baada ya kizaazaa hicho walisema kuwa watasusia shughuli hizo hadi pale watakapopata mwelekeo kamili kutoka kwa KNUT.

“Mpango huu unapaswa kucheleweshwa hadi shule zote zitakapofunguliwa. Utoaji mafunzo wakati wa likizo unawaathiri walimu wengi ambao wamehamishiwa katika maeneo ya mbali,” akasema mwalimu mmoja, ambaye ni miongoni mwa waliofurushwa kutoka kwa Shule ya Msingi ya Kibwezi Township.

Katika Kaunti ya Nakuru, Kaimu Katibu wa KNUT Paul Muiru alilalamikia mpango huo akisema, unaendeshwa bila serikali kuwashirikisha walimu ifaavyo.

Alisema baadhi ya walimu waliopewa mafunzo kuhusu mtaala huo wakati wa majaribio yake wamestaafu, hivyo kufanya utekelezaji wake kuwa mgumu.

Hata hivyo, Waziri wa Elimu George Magoha alisisitiza kuwa serikali haitatishwa na wale wanaopinga mpango huo, kwani imeweka kila mikakati kuhakikisha kuwa umefaulu.

“Hatutarudi nyuma. Tumechukua hatua zote kuhakikisha kuwa mpango huu umefaulu. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi amefaidika,” akasema Prof Magoha, alipozundua mpango huo katika Shule ya Msingi ya Uhuru Gardens, jijini Nairobi. Serikali inalenga kuwapa mafunzo walimu 91,000 kuhusu mfumo huo kabla ya shule za msingi na upili za umma kufunguliwa wiki ijayo.

?WANDERI KAMAU, BENSON AMADALA, WINNIE ATIENO, TITUS OMINDE na PIUS MAUNDU