Bambika

Mtaalamu afichulia wanaume faida za kuoa wanawake wanaowazidi umri

February 7th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

MSHAURI wa masuala ya ndoa Grace Kariuki amekubaliana na kauli yake mwanamuziki Guardian Angel kwamba kuna faida kubwa mwanamume kuoa mwanamke anayemzidi umri.

Bi Kariuki alisema faida huja kwa sababu mwanamke anayemzidi mume umri huwa tayari amepitia mambo mengi ya kisichana na moto unaokuja na ujana.

Mtaalamu huyo aliambia Taifa Leo kwamba katika karne hii, mwanamume kuoa mwanamke anayemzidi umri huwa si uamuzi wa kawaida ambao umezoeleka kwenye jamii, lakini hilo halimaanishi kwamba haufai.

Bila kujali pengo la umri, kuoa mwanamke mkubwa kumzidi mwanamume huleta faida nyingi kwa sababu wanawake wengi wakubwa huwa wanajitambua na kujiamini kwa kile wanachotaka zaidi ni hisia za kuhisi kupendwa.

Mshauri huyo alionya vijana iwapo atamuoa mwanamke mkubwa ambaye hatatimiza mahitaji yake yote na kusababisha moyo kuvunjika, basi ni vyema kuachana na mahusiano hayo.

Mwanamuziki wa Injili Guardian Angel kwenye mahojiano na Clouds FM ya Tanzania, alisema hajutii kumuoa Esther Musila, ambaye anamzidi na umri kwa miaka 20.

Guardian alisema umri haupaswi kuwa sababu kuu ya kutathmini mafanikio ya ndoa.

Alidai mahusiano mengi na yasiyo na tofauti ya kiumri huishia kushindwa kunawiri hata kabla ya miezi sita.

“Umri usiwe kiini cha kuzingatiwa kwenye ndoa. Kuna watu wengi wameoana na kuachana. Kuna watu ambao walioana mimi nikianza ku-date mke wangu na wako na huo umri tunaoongelea na sasa hivi hawako pamoja,” alijitetea Guardian Angel.

“Kujitolea kwangu kwa mke wangu kunazidi umri na maoni ya watu. Kwa sababu mkiingia kwa hicho kitanda ni wewe na mke wako, hamna jamaa wa maoni hapo. Ninacho jali sana ni kuona nina furaha,” aliendelea kujitetea.

Mwanamuziki huyo alifokea wakazi wa Nairobi ambao wamekuwa mstari wa mbele kukosoa ndoa yake.

“Wewe kwanza si wetu, nilikupata tu Nairobi. Sasa hisia zako zinanihusu na nini?” aliuliza staa huyo wa muziki wa Injili.

Kwenye mahojiano hayo, Bi Musila alidai kuwa anapendwa na kamwe hujiona kama mtoto.