Kimataifa

Mtafiti wa virusi atoa ‘ushahidi’ corona iliundwa katika maabara

September 15th, 2020 2 min read

NA MASHIRIKA

MTAALAMU wa maradhi ya kuambukizana ambaye alidai virusi vya corona viliundwa kwenye maabara nchini Uchina, jana alitoa ripoti ya kina ya kuunga utafiti wake.

Dkt Lieng-Meng Yan, ambaye alikuwa mtafiti wa kisayansi katika Chuo cha Afya cha Hong Kong alichapisha ripoti hiyo kwenye mtandao wa zenote, akifafanua jinsi virusi vya corona vinavyoweza kuundwa katika muda wa miezi sita.

Ripoti hiyo ambayo Yan aliandika na waandishi wengine wawili inakanusha madai kwamba Covid-19 ilichipukia kwenye soko moja la nyama jijini Wuhan mwaka jana kama homa ya nguruwe.

Vilevile Yan, kwenye utafiti wake, anasema virusi vya corona huonyesha dalili za kibayolojia ambazo ni tofauti na magonjwa mengine yanayosababishwa na virusi.

Kinaya ni kwamba wanasayansi wengine siku za majuzi nao wameibuka na ripoti zilizoonyesha kwamba virusi vya corona haviwezi kuundwa au kutengenezwa kwenye maabara.

Ripoti ya utafiti wa Yan ilitolewa baada ya kufanya mahojiano na runinga moja nchini Uingereza ambapo alirudia madai yake kuwa serikali ya China ilidhamini mchakato wa kuundwa kwa virusi vya corona katika maabara yao.

“Virusi hivi havitokani na homa ya nguruwe wala havisababishwi na mabadiliko ya kimazingira. Nilipata taarifa za kijasusi kutoka kwa madaktari nchini China na wakanithibitishia kwamba virusi hivyo viliundwa,” akasema Yan.

Mnamo Aprili, Yan alitoroka mji wa Hong Kong na kukimbilia Marekani ili kutoa hamasisho kuhusu virusi vya corona akisema alikuwa akihofia usalama wake.

Mtafiti huyo alikuwa amedai kwamba mkubwa wa afya katika Chuo cha Hong Kong ambaye pia anafanya kazi katika Shirika la Afya Duniani (WHO), alijaribu kumnyamazisha alipojaribu kuzua maswali kuhusu maambukizi ya corona kutoka mtu mmoja hadi mwengine mwaka uliopita.

Yan ambaye ni mwanamke pia alifichua kuwa kabla atoroke kutoka Hong Kong, maelezo yote kuhusu kazi zake za utafiti yalifutwa kutoka kwenye kanzi-data ya serikali ya China.

Hata hivyo, usimamizi wa maabara hiyo nchini China, ulijitokeza na kudai kwamba Yan hakuwahi kufanya utafiti wowote nchini humo na iwapo upo basi hauna msingi wa kisayansi.

Yuan Zhiming, ambaye ni mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Virusi jijini Wuhan, naye amewahi kunukuliwa akikanusha vikali kwamba virusi hivyo vilianzia katika chuo chake.