Habari

Mtahiniwa afariki Nakuru hofu ikizidi kuhusu kemikali za somo la Kemia

November 13th, 2019 1 min read

Na JOSEPH OPENDA

FAMILIA katika kijiji cha Majani Mingi, Rongai, Kaunti ya Nakuru inaomboleza kifo cha kijana wao wa kiume kilichotokea baada ya kufanya mtihani wa somo la Kemia katika maabara.

Mtihani huo ulifanyika Ijumaa wiki jana.

Victor Kiptoo aliyekuwa na umri wa miaka 18 alikuwa akifanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE 2019) katika Shule ya Mseto ya Barina na alifariki Jumatatu jioni akiwa njiani kuelekea hospitalini.

Chanzo cha kifo hakijabainika ingawa familia inakihusisha na somo la utendaji la Kemia.

Baba mzazi wa mhanga, Bw David Ngeno amesema kijana wake alianza kulalama kuhusu maumivu ya kifuo, na kushindwa kupumua vizuri Ijumaa jioni wiki jana baada ya kurejea nyumbani kutoka shuleni.

Mama mzazi ni Bi Nelly Ng’eno.

 

“Nilimpa tembe kadhaa za kuondoa maumivu, lakini tatizo liliendelea. Jumatatu aliamka akiwa hajihisi vizuri na ni hapo ndipo niliamua kumpeleka shuleni. Hali yake ilizidi kuwa mbaya Jumatatu jioni,” amesema Bw Ng’eno ambaye jioni hiyo alimpeleka katika zahanati akafanyiwa vipimo bila kubainisha alichokuwa akiugua.

Hali ya mtoto huyo wa pili katika familia ya watoto sita ilidhoofika zaidi na akapelekwa hospitalini Mogotio wakishuku pengine ilikuwa ni Homa kali ya mapafu.

Hapo Mogotio madaktari walisema alikuwa ameshaaga dunia.

Marehemu pia alikuwa na matatizo ya niumonia.

Mjomba wa marehemu, Bw Ibrahim Silatei kijjana alikuwa akiendelea kupona lakini mauti yakamkumba.

“Pengine aliathirika kutokana na kemikali za maabarani,” amesema Bw Silatei.