Habari Mseto

Mtahiniwa Taita Taveta ajifungua kabla ya kuanza mtihani wa KCPE

October 29th, 2019 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

MTAHINIWA mmoja wa KCPE katika Kaunti ya Taita Taveta amelazimika kufanya mtihani wake hospitalini baada ya kujifungua katika hospitali moja ya eneo hilo.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 14 wa Shule ya Msingi ya Timbila amejifungua katika hospitali ya Taveta mnamo Jumatatu usiku muda wa saa chache kabla ya kuanza kwa mtihani huo.

Wasimamizi wa idara ya elimu katika eneo hilo wamefanya mpango wa kumwezesha mtahiniwa huyo kufanya mtihani wake katika chumba spesheli cha hospitali hiyo.

Akithibitisha kisa hicho, mkurugenzi wa elimu wa kaunti hiyo Bw Samson Wanjohi alisema kuwa tayari mtahiniwa alikuwa anafanya mtihani wake wa kwanza.

“Mwanafunzi yuko katika afya nzuri ya kufanya mtihani. Tumeweka mikakati ya kumwezesha kufanya mtihani bila shida yoyote hadi atakapotoka hospitalini,” amesema Bw Wanjohi.

Aidha, amesema kuwa hakuna kisa kingine kimeripotiwa katika eneo hilo.

Amesema kuwa idara ya elimu inashirikiana na wadau wengine kuhakikisha kuwa shughuli hiyo inafanyika bila tatizo.

Mwaka 2019 jumla ya wanafunzi 8,193 katika vituo 225 wanafanya mtihani wa KCPE katika kaunti hiyo.