Kimataifa

Mtajuta kuturushia makombora, Mkuu wa Jeshi Israel aambia Iran akiapa kulipiza kisasi

April 16th, 2024 2 min read

Na MASHIRIKA

JERUSALEM, Israel

MKUU wa Jeshi la Israel Herzi Halevi ameapa kujibu shambulio la Iran huku miito ya kuitaka Israeli isilipize kisasi ikizidi kuongezeka.

“Hiki kitendo cha kurushwa kwa makombora mengi na droni ndani ya himaya ya Israel kitajibiwa kwa nguvu kali zaidi,” akasema bila kutoa maelezo zaidi.

Jumanne, raia na viongozi nchini Israel walikuwa wakisubiri mwelekeo kutoka kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuhusu iwapo nchi hiyo itafanya mashambulio ya kulipiza kisasi dhidi ya Iran au la.

Msemaji wa jeshi la Israel Admiral Daniel Hagari akiwa amesimama karibu na kombora lililorushwa na Iran kuelekea Israel kusini mwa Israel juzi. Israel sasa inasema italipiza kisasi shambulio hilo. PICHA|REUTERS

Mapema Jumatatu Netanyahu aliongoza kikao cha mawaziri wake kwa mara ya pili ndani ya saa 24 kujadili suala hilo, duru za serikali zilisema.

Ingawa shambulio la Iran halikusababisha vifo, baada ya wanajeshi wa Israeli na washirika wake kudungua makombora hayo, limeibua hofu ya kuenea kwa vita vinavyoendelea Gaza. Aidha, kuna wasiwasi kwamba huenda vita kamili vikazuka kati ya Israel na hasidi wake wa muda mrefu Iran.

Naibu Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Iran Ali Bagheri Kani aliiambia runinga ya kitaifa Jumatatu jioni kwamba Iran itajibu mara moja shambulio kutoka Israel.

“Iran itajibu ndani ya sekunde chache, haitasubiri kwa siku zingine 12 kufanya shambulio,” akasema.

Naye Rais wa Iran Ebrahim Raisi alisema Jumanne kwamba taifa lake litajibu shambulio lolote dhidi ya vituo vyake.

“Tunatangazaa wazi wazi kwamba hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi ya vituo vya Iran zitakabiliwa kwa hatua kali dhidi ya mvamizi yeyote,” Raisi akaambia kiongozi wa Qatari Emir Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani.

Lakini uwezekano wa Israel kufanya shambulio la kulipiza kisasi limewatia hofu raia wa Iran ambao wanakumbwa na makali ya kiuchumi na kudhibitiwa kisiasa na kijamii tangu maasi yaliyotokea kati miaka ya 2022 na 2023.

Iran ilishambulia Israel Jumamosi kujibu shambulio lililotekelezwa na Israel katika ubalozi wake jijini Damascus nchini Syria mnamo Aprili 1 mwaka huu.

Baadaye ilisema haingetaka kuendeleza mashambulio zaidi.

“Tunajua kuwa ulimwengu unatutazama kuona hatua ambayo tutachukua,” wizara ya masuala ya kigeni ya Iran ikasema kwenye taarifa.

Mnamo Jumapili Rais Joe Biden alimfahamisha Netanyahu kwamba Amerika haitashiriki katika hatua zozote za Israeli kujibu shambulio la Iran, kulingana na maafisa wa Amerika.

Tangu vita vilipoanza Gaza Oktoba mwaka jana, mapigano yametokea katika ya Israel na makundi washirika wa Iran, yaliyoko Lebanon, Syria, Yemen and Iraq.

Mapema Jumatatu nchi za bara Uropa, ambazo ni washirika wa Israel, ziliihimiza kujizuia na kutotekeleza mashambulio ya kulipiza kisasi Iran.

Nchini hizo; Uingereza, Ufaransa, Ujerumani ziliendeleza miito iliyotolewa na Amerika pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres ya kuwataka viongozi wa Israeli kujiepusha na hatua hiyo itakayozidisha mapigano katika eneo la Mashariki mwa Kati.